Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa pamoja na mwenzake wa kijeshi, wanatarajiwa kusisitiza kuhusu wasiwasi wa serikali yao kutokana na harakati za Kremlin, Afrika magharibi wakati watakapokutana na wenzao wa Russia, Paris Ijumaa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters kumekuwa na hali ya mivutano kati ya mataifa hayo na kuendelea kwa tofauti juu ya suala la Ukraine na katika miezi ya karibuni kuhusu mamluki wanaodaiwa kutoka Russia, walioko kwenye baadhi ya mataifa ya Afrika magharibi ambako vikosi vya Ufaransa vinakabiliana na wanamgambo wa kiislamu.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian, amedai kwamba mamluki hao wanaendesha shughuli zao kwa niaba ya Russia.
Taarifa ya pamoja kutoka kwa mawaziri hao wa Ufaransa imesema kwamba kikao cha Ijumaa kitajadili hali ya kisiasa na kijeshi katika mizozo ya kikanda na kimataifa, haswa suala la Ukraine na kwenye eneo la SAHEL, ambapo ufaransa imeelezea wasiwasi wake.
Vyanzo vya kidiplomasia pamoja na kiusalama vimeiambia Reuters kwamba utawala wa kijeshi uliofanywa mapinduzi ya serikali nchini Mali unakaribia kuandikisha mamluki kutoka kampuni ya Wagner ya Russia.
Ufaransa kwa upande wake imejitahidi kutumia njia ya kidiplomasia kuzuia hatua isiyo endana na uwepo wake kwenye taifa hilo lililokuwa koloni lake.
Mwezi Septemba mwaka jana, mawaziri wa mambo ya nje na jeshi wa Ufaransa waliahirisha ziara yao mjini Moscow wakati baadhi ya mataifa ya Ulaya yalipokuwa yakitaka majibu kutoka Russia baada ya Ujerumani kuthibitisha kwamba mkosoaji mkubwa wa Russia Alexei Navalny, aliwekewa sumu na serikali.