Maelfu ya vijana wanaharakati wa mazingira, wanajitayarisha kufanya maandamano mjini Glasgow, Scotland hii leo, kulalamikia kile wametaja kama ukosefu wa viongozi wanaohudhuria kongamano kuhusu mazingira COP26, kuchukua hatua dhabiti kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Waandamanaji wanatarajiwa kote mjini humo kuangazia ukosefu wa uwiano kati ya kiwango cha hewa chafu inayoingia katika mazingira na namna mabadiliko ya hewa yanavyoathiri ulimwengu.
Waandalizi wa maandamano hayo wamesema kwamba wanatarajia watu kadhaa kujitokeza katika maandamano ya saa tatu wakati wa siku ya vijana katika kongamano hilo la COP26.
Mwanaharakati wa mazingira Mitzi Joelle kutoka Ufilipino amesema kwamba wanaona viongozi wakitoa hotuba nzito nzito namba ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa bila kuona hatua zozote zikichukuliwa.
Wanaharakati wanasema kwamba wanataka kuona viongozi wakipunuza sana kiwango cha hewa ya Carbon inayoingia katika mazingira.
Wataalam wanasema kwamba ahadi iliyotolewa na viongozi wa ngazi ya juu kutoka nchi 100, katika kongamano hilo, kupunguza gesi ya Methane inayoingia katika mazingira kwa kiasi cha asilimia 30, italeta mabadiliko madogo sana kwa kuongezeka kwa hali ya joto duniani.