Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 10:05

10 wauawa katika mashambulizi Burkina Faso


Mwanajeshi wa Burkina Faso akipiga doria nje ya kambi ya wakimbizi wa ndani
Mwanajeshi wa Burkina Faso akipiga doria nje ya kambi ya wakimbizi wa ndani

Watu 10 wameuawa katika shambulizi lililotokea Kaskazini mwa Burkina Faso jumatatu asubuhi.

Chanzo cha habari ndani ya serikali na maafisa wa usalama kimesema kwamba watu wengine 4 hawajulikani walipo na inahofiwa kwamba wametekwa nyara.

Watu waliokuwa wamejihami kwa silaha, na ambao hawajatambuliwa kufikia sasa, wameshambulia kundi la raia waliokuwa wanasukuma mikokoteni yao kuelekea sokoni katika mji wa Markoye, eneo la Sahel, waliposhambuliwa.

Sehemu hiyo, iliyo mpakani na Mali na Niger, inadhibitiwa na wapiganaji wa kiislamu, wanaotekeleza mashambulizi kila mara licha ya kuwepo wanajeshi wa kupambana na ugaidi Pamoja na wanajeshi wa Ufaransa.

Burkina Faso imeadhimisha miaka 61 tangu kuundwa kwa jeshi lake. Maadhimisho yameangazia namna ya kupambana na ugaidi.

Rais Roch Kabore amesema kwamba “tutashinda hali hii kwa Pamoja ama tushindwe kabisa”

Makundi ya kiislamu yamekuwa yakiteleza mashambulizi katika eneo la Sahel barani Afrika na kuua maelfu ya watu huku wengine kadhaa wakilazimika kutoroka makwao nchini Burkina Faso, Mali na Niger.

Kulingana na shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, zaidi ya watu milioni 1.3 wamekosesha makao nchini Burkina Faso katika mda wa miaka miwili.

Wizara ya usalama ya Burkina Faso imesema kwamba maafisa wa polisi watano wameuawa Jumapili katika shambulizi lililotokea kaskazini mwa nchi hiyo, na karibu washambuliaji 15 waliuawa katika makabiliano kati ya maafisa wa usalama na wapiganaji.

Shirika la habari la serikali limeripoti kwamba wanawake wawili na mtoto waliuawa jumapili mkokoteni wao ulipogonga bomu la kutegwa ardhini katika sehemu ya Ouindigui.

XS
SM
MD
LG