Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 20:23

Uganda yaidhinisha $334.5M kujenga barabara DRC, wachambuzi wasema ni mbinu ya kuishambulia ADF


Rais Félix Tshisekedi (kushoto) wa DRC na rais wa Uganda Yoweri Museveni (kulia) wakisimama kwenye jiwe la msingi la kujenga barabara kati ya Kasindi na Mpondwe. 16 juin 2021. (Twitter/Présidence RDC)
Rais Félix Tshisekedi (kushoto) wa DRC na rais wa Uganda Yoweri Museveni (kulia) wakisimama kwenye jiwe la msingi la kujenga barabara kati ya Kasindi na Mpondwe. 16 juin 2021. (Twitter/Présidence RDC)

Jee milipuko miwili ya mabomu karibu na Kampala kati kati ya mwezi wa Oktoba ndiyo yalisababisha baraza la mawaziri wa Uganda kuidhinisha Jumatatu Oktoba 25, 2021 makubaliano kati ya Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kushirikiana katika ujenzi wa barabara mashariki mwa DRC?

Hilo ndilo swala wachambuzi wanauliza baada ya baraza hilo kuidhinisha mkataba huo ulosainiwa mwezi March 2021, ili kujenga barabara ndani ya DRC kwa ajili ya kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Mkutano hio umefanyika pia siku moja baada ya Rais Museveni kukutana na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Bintou Keita, pamoja na mkuu wa kikosi cha jeshi la umoja wa mataifa nchini Congo MONUSCO, katika ikulu ya rais ya Entebbe, Uganda.

Walijadiliana kuhusu usalama katika kanda ya maziwa makuu.

Mkutano huo umefanyika mwaka mmoja baada ya kufanyika mkutano kama huo kuhusu namna ya kuhakikisha kuna amani Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Mkataba huo utagharimu dola za kimarekani milioni 334.5 na kila nchi itagharamia nusu ya bajeti hiyo.

Baadhi ya wachambuzi wanasema mradi huu ni wa kuisaidia DRC kurejesha hali ya utulivu mashariki mwa DRC.

Wadadisi wanasema hii ni hatua ya mwanzo ya serikali yake Museveni, kabla ya kuanza vita dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces ambao wamehangaisha sehemu za mshariki mwa Uganda kwa mda mrefu.

“Sio kwamba Museveni ana nia sana ya kuendeleza DRC kiuchumi, lakini anataka kudhibithi usalama sio tu ndnai ya DRC bali pia ndani ya Uganda. Lenye linatangulia zaidi sio barabara. Ni uslama wa nchi ya Uganda” amesema Richard Tuta, mchambuzi wa usalama katika kanda ya maziwa makuu katika mahojiano na sauti ya Amerika wakati wa kipindi cha kwa Undani.

Barabara zitakazojengwa ni pamoja na barabara kuu yenye urefu wa kilomita 89 inayounganisha Bunagana, Rutshuru na Goma, barabara yenye urefu wa kilomita 54 kutoka Beni hadi Butembo na barabara yenye urefu wa kilomita 80 kutoka Kasindi hadi Beni.

Kuna ripoti kwamba tayari Uganda imeshatuma wanajeshi wake ndani ya DRC kwa matayarisho ya kuanza ujenzi wa barabara hizo.

Kabla ya kuanza ujenzi wa barabara katika sehemu ambayo imekumbwa na mapigano, ni lazima jeshi la Uganda UPDF lihakikishe kwamba kuna usalama wa kutosha kwa wafanyakazi wanaofanya kazi ya ujenzi wa barabara hizo.

Kundi la wapiganaji la ADF, ambalo limetangaza kushirikiana na kundi la Islamic state ISIS, limeshutumiwa kwa kutekeleza mashambulizi na kusababisha vifo, uharibifu mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Kundi hilo vile vile limeshutumiwa kwa kupiga risasi na kuwaua viongozi wa ngazi ya juu nchini Uganda wakwiemo wabunge, viongozi wa dini ya kiislamu, mwendesha mashtaka, aliyekuwa msemaji wa polisi Felix Kaweesi, miongoni mwa wengine.

Kundi hilo vile vile lilitajwa katika jaribio la kutaka kumuua aliyekuwa kamanda mkuu wa jeshi Generali Katumba Wamala, katika shambulizi lililopelekea kifo cha binti wake.

Uganda imelaumu ADF kwa mashambulizi mawili ya mabomu ambayo yametokea Uganda wiki iliyopita na kuua watu wawili.

Eneo ambalo mlipuko wa bomu ulitokea mjini Kampala, Uganda, Oct. 24, 2021.
Eneo ambalo mlipuko wa bomu ulitokea mjini Kampala, Uganda, Oct. 24, 2021.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amekuwa akitafuta uungwaji mkono wa viongozi wa nchi zakanda ya Maziwa Makuu katika juhudi za kuhakikisha kwamba DRC ina utulivu na makundi ya wapiganaji yameshindwa nguvu.

Zaidi ya watu milioni 5 wameathiriwa na vita vya kundi la ADF nchini DRC.

Uganda imewapa makao zaidi ya wakimbizi nusu milioni kutoka nchi jirani, wanaotoroka mapigano, hasa DRC.

“Magaidi wamekuwa wakifanya mambo wanayotaka mashariki mwa DRC kwa mda mrefu. Hili haliwezi kukubalika “amesema Museveni katika mkutano huo.

Uganda ni mwenyeji wa wakimbizi zaidi ya 400,000 kutoka DRC. Zaidi ya watu 700, 000 wamekoseshwa makao ndani ya DRC kutokana na vita vya ADF.

“Baraza la usalama la umoja wa mataifa linastahili kuandaa kikao kujadili hali ya usalama DRC na kusisitiza kwamba mashariki mwa DRC imekuwa handaki la kuzalisha makundi ya wapiganaji. Ni tatizo ambalo linaendelea kuongezeka na linastahili kupata suluhu la haraka” amesema Museveni.

Tuta anasema kwamba kuwepo kwa kundi la ADF nchini Congo inayumbisha Uganda kwa namna nyingi kiuchumi, kisiasa na kiusalama na ni lazima rais wa Uganda Yoweri Museveni atumie mbinu zote za kidiplomasia kuishawishi serikali ya DRC kukubali kushirikiana kumaliza nguvu waasi hao.

“Waasi wa ADF wanakaa DRC. Wanaingia Uganda na kutekeleza mashambulizi kisha wanarudi DRC kujificha. Ndipo Museveni aweze kukabiliana nao, ni lazima awafuate katika sehemu zao wanazofanyia mipangilio. Kule ndipo kuna mazingira yanayowafaa. Lazima wanajeshi wa Uganda waingie kule kuharibu hayo mazingira," amesema Tuta.

Ameongeza kusema kwamba “sababu kubwa ya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kutaka ibembelezwe katika kuruhusu wanajeshi wa Uganda kuingia huko kupambana na waasi wa ADF ni kwmaba kila nchi inatumia kile ilicho nacho katika kueneza uhusiano wa kimataifa. Na hivi sasa katika kumbana Museveni kuwasikiliza ni kuwaambia kwamba ukitupa hiki, tutakuruhusu upambane nao”.

Wanajeshi wa Uganda UPDF, wamekuwa wakishika doria kwenye mpaka wa Uganda na DRC, tayari kukabiliana na waasi wa ADF endapo watavuka mpaka na kuingia Uganda.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG