Muungano wa wanajeshi wa Afrika wanaolinda amani Somalia, umekanusha madai kwamba ulishiriki katika mapambano ya wiki hii katik amji wa Guri-el, jimbo la Galmudug kati ya makundi ya wapiganaji na wanajeshi wa serikali, na kupelekea vifo vya watu 120.
Wapiganaji wa kundi la kiislamu la Ahlu Wal Jamaa, walipigana na wanajeshi wa Somalia na wanajeshi wa jimbo la Galmudug, kati ya jumapili na jumatano.
Lakini ripoti zilienea kwamba wanajeshi wa Amisom walishiriki katika mapigano hayo mabaya na walitoa msaada wa silaha kwa wanajeshi wa serikali.
Amisom wamesema madai hayo ni ya uongo, sumu na ya kuharibu sifa ya jeshi hilo, na kwamba lengo lake ni kuharibu uhusiano kati yake na watu wa Somalia.