Uingereza imeanza matumizi ya chanjo dhidi ya vurusi vya Corona, inayotengenezwa na kampuni ya AstraZeneca.
Chanjo hiyo imeanza kutolewa leo Jumatatu.
Chnajo ya AstraZeneca ni ya bei nafuu na rahisi kusafirishwa ikilinganishwa na chanjo ya Pfizer BioNTech, kwa sababu haihitaji kusafirishwa katika mazingira yenye nyuzi joto za chini sana.
Chanjo hiyo inaanza kutolewa Uingereza wakati nchi hiyo inaendelea kuripoti ongezeko kubwa la maambukizi ya aina mpya ya virusi vya Corona ambayo inaripotiwa kuambukiza kwa kasi sana kuliko aina ya kwanza.
Waziri mkuu Boris Johnson ameonya kwamba huenda masharti ya watu kusalia nyumbani kwao yakatangazwa tena ili kudhibithi maambukizi.
India pia imeidhinisha matumizi ya chanjo hiyo kwa matumizi ya dharura japo maadhi ya wataalam wa afya wameelezea wasiwasi kwamba hatua ya kuidhinisha chanjo hiyo imeharakishwa sana.
India imeripoti kwamba zaidi ya watu 16,500 wameambukizwa virusi vya Corona katika saa 24 zilizopita.
India ni ya pili kwa idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona kote duniani baada ya Marekani.
Kulingana na chuo kikuu cha Johns Hopkins watu milioni 1.03 wameambukizwa virusi vya Corona nchini India. Watu milioni 20.6 wameambukizwa virusi hivyo nchini Marekani.