Hatua hii inatokana na ripoti za kuwepo aina mpya ya virusi vya Corona ambavyo vinasambaa kwa haraka sana kuliko aina ya kwanza.
Kituo cha kuzuia na kudhibithi magonjwa nchini Marekani kimesema katika taarifa kwamba abiria wanaoingia Marekani kutoka Uingereza lazima wawe na vyeti kuonyesha kwamba hawajaambukizwa virusi hivyo, kuanzia Jumatatu wiki ijayo.
Amri hiyo ni kinyume na taarifa iliyolewa na utawala wa rais Donald Trump iliyosema kwamba hakukuwepo mpango wa kuwalazimisha wasafiri kutoka Uingereza kupimwa ili kutambua iwapo wameambukizwa virusi vya Corona.
Nchi kadhaa zimefungwa mipaka yake kwa wasafiri kutoka Uingereza baada ya ripoti za kuwepo aina mpya ya virusi vya Corona nchini humo.
Baadhi ya mashirika ya ndege ya Marekani tayari yanataka wasafiri wake kupimwa virusi vya Corona kabla ya kusafiri.
Mashirika ya ndege yanayosafiri kutoka London hadi uwanja wa John F. Kennedy hapa Marekani, kama Delta, British airways na Virgin Atlantic, yamekubali ombi la gavana wa New York Andrew Cuomo, kuhakikisha kwamba wasafiri wote wamepimwa virusi vya Corona, saa 72 kabla ya kuanza safari kutoka Uingereza.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC