Mechi za ligi za mpira wa kikapu Marekani za wanawake na wanaume - WNBA na NBA - ziliahirishwa Jumatano usiku kupinga kitendo cha kijana Mmarekani mweusi kupigwa risasi na polisi katika mji wa Kenosha, Wisconsin.
Kuahirishwa kwa mechi hizo kulifuatia hatua ya kwanza iliyochukuliwa na timu ya Milwaukee Bucks kugomea mechi yao ya tano katika ligi ya mtoano dhidi ya Orlando Magic. Orlando ilifika uwanjani, lakini Bucks hawakutokea.
Saa chache baadaye NBA ilitoa taarifa ikisema mechi zote zilizokuwa zichezwe Jumatano usiku ikiwa ni pamoja na Houston Rockets dhidi ya Oklahoma City Thunder, na Los Angeles Lakers dhidi ya Portland Trailblazers zimeahirishwa.
Muda si mrefu baada ya hapo WNBA nayo ikatangaza kuahirisha mechi zake tatu ambazo zilikuwa zichezwe usiku.
Hatua ya NBA kuahirisha mechi hizo tatu ina maana Milwaukee Bucks ambayo ilichukua hatua ya kwanza haitapoteza mechi yake iliyokuwa icheze na Orlando Magic na kwamba itaendelea kuwa inaongoza mechi 3-1.
Hatua ya NBA leo inafuatiliwa kupigwa risasi kwa kijana mmoja Mmarekani Jacob Blake katika jimbo linakotokea timu hiyo ya Bucks, Wisconsin. Blake alipigwa risasi mara saba na polisi wakati anajaribu kuingia ndani ya gari lake baada ya mvutano na polisi. Watoto wake watatu walikuwa ndani ya gari hiyo. Blake yuko hospitali mpaka sasa na madaktari wanasema huenda asiweze kutembea tena kwa miguu yake mwenyewe.
Kupigwa risasi kwa Blake ni tukio jingine miongoni ya kadha baina ya mwaka jana na mwaka huu, matukio ambayo yamesababisha hasira miongoni mwa wamarekani weusi na wazungu kuhusu kile ambacho wanasema ni "uonevu" wa polisi dhidi ya wamarekani weusi.
Kocha wa timu ya Los Angeles Clippers, Doc Rivers, alizungumza kwa hisia kali Jumanne usiku baada ya mechi ya timu yake na Dallas Mavericks akisema haelewi kwa nini "naipenda nchi hii, lakini nchi hii hainipendi"
Hatua ya Milwaukee Bucks kugomea mechi na hatimaye NBA kuahirisha mechi nyingine mbili itachukuliwa kama ya kihistoria Marekani ambako michezo mara nyingi imetumiwa kupigania haki za raia.