Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 08:09

Trump amwachisha kazi mkurugenzi wa FBI


Aliyekuwa mkurugenzi wa FBI James Comey.
Aliyekuwa mkurugenzi wa FBI James Comey.

Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, Marekani (FBI) ameachishwa kazi siku ya Jumanne na rais Donald Trump.

Taarifa kutoka ikulu imesema Trump alichukua hatua hiyo baada ya kupata ushauri kutoka kwa mwanasheria mkuu, Jeff Session na naibu wake, Rod Rosenstein.

"Leo rais Donald Trump amemjulisha mkurugenzi wa FBI James Comey kwamba ameachishwa kazi na kuondolewa madarakani," ilisema taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na msemaji wa ikulu, Sean Spicer Jumanne jioni.

Taarifa hiyo ileleza kuwa shughuli za kumtafuta mkurugenzi mpya wa idara hiyo zilikuwa zimeshaanza.

Kuachishwa kazi kwa Comey kulipokelewa kwa mshangao na baadhi ya wabunge na maseneta.

Wiki jana, Comey alihojiwa na kamati ya seneti kuhusu tuhuma kwamba huenda Russia iliingilia kuvuruga uchaguzi wa Marekani wa Novemba mwaka uliopita.

Aidha mkurugenzi huyo wa zamani amekuwa akikabiliwa na tuhuma kwamba uamuzi wake wa kutangaza kwamba idara yake ilikuwa imefungua uchunguzi kuhusu barua pepe za Hillary Clinton mnamo siku za mwisho za kampeni, ulisababisha kushindwa kwa mwanasiasa huyo wa chama cha Demokratik.

Comey aliteuliwa na rais Barack Obama mnamo mwaka wa 2013 na alitarajiwa kuhudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka isiyozidi 10. Hata hivyo, rais Trump ana mamlaka ya kumwachisha kazi mkurugenzi wa FBI wakati wowote.

Imetayarishwa na mwandishi wetu BMJ Muriithi, Washington, DC

XS
SM
MD
LG