Kwa mujibu wa rais wa bunge la Kasai Francois Kalamba, wanamgambo hao walishambulia msafara wa magari ya polisi uliokuwa unasafiri kutoka mji wa Tshikapa kuelekea mji mkuu wa jimbo la Kasai wa Kananga waliposhambuliwa Ijumaa na wanamgambo hao.
Kalamba amesema walioshuhudia wameeleza kuwa wanamgambo waliwaachilia huru maafisa sita kwa vile walikuwa wanazungumza lugha ya Tshiluba inayotumika eneo hilo.
Anasema wanamgambo hao ambao kawaida huwa na mapanga, waliiba bunduki na silaha za polisi na kukimbia pamoja na magari yao.
Uasi katika eneo la kati ya DRC ulianza mwezi Agosti mwaka jana na umeenea katika majimbo kadhaa ya eneo hilo.
Hata hivyo siku ya Jumamosi wizara ya mambo ya ndani ya serikali kuu imetangaza kwamba kuna wanamgambo 400 wamejisalimisha wiki hii katika jimbo hilo la Kasai.