Waziri wa Sheria Jeff Sessions anakabiliwa na shutuma za kutosema ukweli mbele ya kamati ya sheria ya Seneti kwamba alikutana na balozi wa Russia wakati wa mahojiano ya kuidhinishwa kuwa mwanasheria mkuu.
Kwa hivyo anashutumiwa kudanganya wakati wa mahojiano na kamati ya sheria ya Baraza la Seneti. Hata hivyo mwenyekiti wa kamati hiyo Charles Grassley amemtaka Sessions kutoa maelezo kamili kwa maandishi juu ya kilichozungumzwa wakati alipokutana na balozi wa Russia.
Grassley alikataa matakwa ya Wademokrati ya kumwita tena mbele ya kamati hiyo ili kueleza kwa nini hakueleza juu ya mkutano wake na balozi wa Russia alipokuwa anahojiwa.
Sessions amesema Alhamisi kwamba amejitoa katika uchunguzi wa serikali kuu juu ya Russia kuingilia kati uchaguzi wa rais wa mwaka 2016. Amesema kuwa watu wasichukulie kujiondoa ni ishara ya kuthibitisha kwamba uchunguzi wa namna yoyote umeshaanza.
Rais Trump na maafisa wa White House, lazima pia wapambane na matokeo yasio tarajiwa kuhusu taarifa za mikutano ya balozi wa Russia aliofanya kwenye Jengo la Trump Tower huko New York, Disemba na mkwe wa Trump, Jared Kushner, na aliyeondoshwa katika wadhifa wa mshauri wa usalama, Michael Flynn.
Sessions alikuwa Seneta wa kwanza madarakani kumuunga mkono Trump. Seneta huyu amewahi kutuhumiwa kwa ubaguzi mwaka 1986 baada ya wanasheria wanne waliokuwa wakifanya kazi chini yake kuleta malalamiko dhidi yake.
Rais Donald Trump kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani amenukuliwa akisema Jeff Sessions hakufanya jambo lolote baya. Na rais pia amesema hakuna sababu kwa Sessions kujiondoa katika uchunguzi unaofanywa dhidi ya Russia.
Lakini siku ya Ijumaa Sessions alitangaza kuwa hatajihusisha na uchunguzi wowote utakaofanyika kuhusu kampeni za Trump na Russia.
Taasisi ya kutetea haki za kiraia, American Civil Liberties Union, imetaka Sessions achunguzwe kama amefanya kosa la kudanganya akiwa chini ya kiapo.
Wademokrat kwenye kamati ya sheria ya bunge wametaka idara ya upelelezi wa jinai FBI ifanye uchunguzi iwapo Sessions amevunja sheria kwani wanadai kwamba aliiambia Seneti hakuwa na mawasiliano na Russia wakati aliwahi kukutana na balozi.
Wakati wataalam wa sheria wanasema Sessions atakuwa na makosa ikiwa tu atagundulika alidanganya kwa makusudi na si vinginevyo. Kwa mfano akiwa atasema hakukusudia kuficha kitu bali alisahau kadhia yote hiyo itabadilika.
Warepublikan wenzake Sessions, akiwemo Jason Chafetza na Kevin McCarthy, ambao ni wabunge wamemtaka ajiondoe na uchunguzi wowote kuhusu Russia, na Sessions tayari ameshafanya hivyo.
Wachambuzi wa kisiasa na kisheria bado wanasema kwamba huu ni mwanzo tu wa sakata hilo la kashfa ya udukuzi ya Russia ndani ya serikali ya Rais Donald Trump.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Sunday Shomari, Washington, DC