Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 00:21

Mashariki ya Kati, Ulaya zakerwa na amri ya Trump


Bunge la Iraq
Bunge la Iraq

Kamati ya Bunge la Iraqi imeitaka serikali ya nchi hiyo Jumapili “kujibu” amri yenye utatanishi iliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump ikiwazuia kwa siku 90 wahamiaji kutoka nchi saba za Kiislamu.

Serikali ya Iraq bado haijatoa tamko la wazi juu ya amri ya kiutendaji iliyotolewa na Trump ikiwazuia raia wa Iraq, Syria, Iran, Sudan, Libya, Somalia na Yemen kuingia Marekani.

Amri ya kiutendaji iliyotolewa na Trump pia imepiga marufuku kwa muda usiojulikana kuingia kwa wakimbizi wa Syria nchini na kuzuia kwa siku 120 wakimbizi wengine kuingia nchini.

Rais Trump na Makamu wake Mike Pence
Rais Trump na Makamu wake Mike Pence

​Lakini maafisa wa serikali huko Baghdad wanasema wataendelea kuishawishi serikali ya Marekani kuondoa kipingamizi hicho, au angalau kulegeza kidogo taratibu zinazo waathiri wananchi wa Iraq.

Pia wanampango wa kuitahadharisha White House kwamba kusitisha kwa muda kuingia nchini wahamiaji kunaweza kudhoofisha ushirikiano uliokuwapo katika vita dhidi ya kikundi cha kigaidi cha Islamic State.

Serikali za nchi nyingine za kiarabu zimekaa kimya katika kujibu hadharani suala hilo la upigaji marufuku wakipendelea kuishawishi kwa siri Washington kulegeza amri hiyo.

Viongozi wa shirikisho la Falme 7 za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia watazungumza na Rais Trump kwa simu Jumapili na kwa mujibu wa afisa huko Dubai, ambaye aliongea na VOA kwa sharti jina lake lisitajwe, uongozi utamtahadharisha rais wa Marekani kutokuiongeza falme yeyote katika orodha ya nchi zilizopigwa marufuku.

White House yatoa onyo

Maafisa wa White House Jumamosi wameonya kuwa nchi nyingine zinaweza kuongezwa katika jumla ya orodha ya nchi 7 zilizoko katika amri hiyo, ikiwa pia ni hatua ya“Kulilinda taifa kutokana na magaidi wa kigeni kuingia Marekani.”

Majaji wa mahakama kuu Marekani wamezuia amri inayokataza watu kusafiri, inayowabana wakimbizi na wenye viza- wakiwemo wakazi wa kudumu wa Marekani- waliozaliwa katika moja ya nchi zilizoorodheshwa katika amri hiyo.

Majaji walitoa uamuzi papo kwa papo wakipunguza makali ya amri hiyo wakati mawakili wa haki za binadamu wamesema wana mashaka iwapo katazo hili liko kikatiba.

Iran Jumamosi ilitangaza kuwa itapiga marufuku raia wa Marekani kuingia katika Jamhuri ya Kiislamu ikilipiza kisasi kuzuiwa kwa raia wake.

Katika tamko lake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameiita amri ya Trump “Ni tusi kwa ulimwengu wa Kiislamu.” akiongezea kuwa kizuizi hiki “ni zawadi kubwa kwa wenye itikadi potofu na wale wanaowasaidia.”

Tehran imeonya kuwa kizuizi kilichowekwa na Marekani hakiwezi kuwafanya Marekani kuwa salama zaidi. Wizara imesema hatua iliyochukua kulipa kisasi itaendelea mpaka pale Marekani itapoondoa vikwazo hivyo.
Juhudi za kuzuia magaidi

Maafisa wa White House wamesema kuwa kupigwa marufuku raia kutoka Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen ni sehemu ya juhudi za kuzuia magaidi kuingia Marekani.

Na Rais Trump na wasaidizi wake wanasema wale wanaopinga amri ya kiutendaji wana wasiwasi wa bure.

“Hiki sio kikwazo kilichokusudiwa kwa waislamu,” rais aliwaambia waandishi wa habari katika ofisi yake. “Tulikuwa tumejiandaa vizuri. Inafanya kazi vizuri amri hii. Umeona katika viwanja vya ndege, na kila pahala. Inafanya kazi vizuri kabisa.”

Fikra za viongozi wa Magharibi

Lakini hiyo sio fikra ya viongozi wa Magharibi. Wakati serikali za nchi za Kiarabu zimechagua kutumia njia ya kimya kimya kuishawishi Marekani juu ya kuzuia wasafiri, amri ya Trump imeibua wimbi la ghadhabu sio tu Mashariki ya Kati lakini hata Ulaya ambapo viongozi wake wamelaani kitendo cha kupiga marufuku wahamiaji na wakimbizi.

Ufaransa

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema ili kuihami demokrasia “inahitaji kufuata nguzo za msingi” kati ya hizo nikuwakaribisha wakimbizi. “Na pale ambapo yeye (Trump) anakataa kupokea wakimbizi, wakati Ulaya imetekeleza wajibu wake, lazima tulielezee hilo,” Kiongozi wa Ufaransa amesema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na Ujerumani hata hivyo wameeleza masikitiko yao baada ya mkutano wao Paris.

“Kuwakaribisha wakimbizi ambao wanakimbia vita ni sehemu ya wajibu wetu,” Jean-Marc Ayrault wa Ufaransa amesema baada ya mkutano na waziri mwenzake wa Ujerumani, Sigmar Gabriel.

Ujerumani

Chansella Angela Merkel
Chansella Angela Merkel

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amekosoa amri ya Trump juu ya kuwazuia wahamiaji. Amesema kuwa “sio haki kuwashuku kwa jumla kundi fulani la watu wenye asili moja au imani moja” kwa ajili ya kupambana na magaidi wachache.

Msemaji wa Merkel amesema, “Chansela anasikitishwa na amri ya Marekani juu ya kupiga marufuku wakimbizi na raia wa nchi nyingine kuingia nchini.

Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, ambaye alikutana na Trump huko Washington Ijumaa, alikuwa muangalifu alipokuwa anatembelea Uturuki siku moja baada ya ziara ya Marekani, akijizuia kutokosoa kizuizi hicho kwa Waislamu.

Lakini Jumapili alibadilisha msimamo wake akitoa tamko katikati ya usiku akisema hakubaliani na sera hiyo ya Marekani ya kuzuia wahamiaji na wakimbizi.

Kiongozi huyo wa Uingereza amesema kuwa ataiomba Marekani, kama amri hiyo itawaathiri Waingereza ambao wana uraia pacha na nchi yeyote iliyorodheshwa katika amri ya kiutendaji ya Rais Trump.

XS
SM
MD
LG