Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Jamii Media Limited, maarufu kama Jamii Forums, Maxence Melo amefikishwa hatimae mbele ya mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar es salaam siku ya Ijuma.
Mwandishi wa VOA Dina Chahali anaripoti kwamba Melo alisomewa mashtaka matatu yanayomkabili, likiwemo kuzuia kutoa taarifa za upepelezi kwa jeshi la polisi huku akijua kuwa jeshi hilo linaendelea na upelelezi.
Mkurugenzi huyo alikana mashtaka hayo yote.
Wakili wake Gebra Kabole ameiambia Sauti ya Amerika kuwa mteja wake amesomewa mashtaka hayo mbele ya mahakimu watatu tofauti wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jambo ambalo limezuia mteja wake kupata dhamana.
Hii ni baada ya kushindwa kutimiza masharti katika shtaka la mwisho kutokana na kuchelewa kwa baadhi ya nyaraka, alisema.
“Kama walikuwa na nia ya kuliendesha kistaarabu ilikuwa iwe shtaka moja wametawanya najua wanamamlaka,” aliongeza.
Ameongeza kusema inapofikia hatua kama hiyo mwisho wa siku inabidi kufuata utaratibu wa kisheria.
Mashtaka mengine ni lililojirudia la kuzuia na kuharibu data ambazo jeshi la polisi wamekuwa wakitaka kwa ajili ya uchunguzi. Jingine nikushindwa kwake kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na kuharibu uchunguzi, na Kuendesha mtandao wa kijamii bila kusajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi kifungu cha 79 cha sheria za Epoka.
Kwa upande wa mwanasheria mwandamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, Johanes Karugulaa amesema Melo ameshtakiwa kwa kufanya biashara ya kutoa huduma ya jamii kwa kutumia anwani za kielektronia, na majina ya domain bila ya kufuata sheria za nchi.
“Mtu yoyote anaemiliki mtandao wa kijamii, uwe wa kiitikadi, wa kiwana harakati, wa kisiasa au kidini; endapo atabainika anakiuka sheria za nchi hatutamvumilia tutaufunga mara moja huo mtandao,” alifafanua mwanasheria huyo.
Maxence Melo alikamatwa kwa mara ya kwanza Desemba 13 mwaka huu na alikuwa akishikiliwa katika kituo kikuu cha polisi jijini dar es salaam kabla ya leo kufikishwa mahakamani huku taarifa zikieleza kwamba tayari polisi wamefanya upekuzi katika ofisi za mmiliki huyo wa jamii Forums na nyumbani kwake pamoja na kuondoka na nyaraka kadhaa za kampuni yake.