China imeeleza siku ya Jumatatu kua imekerwa sana na maoni ya Rais Mteule wa Marekani Donald Trump akihoji iwapo Marekani iendelee na sera yake “China moja” kwa sharti kuwa serikali ya China itoe fursa zaidi za kibiashara.
Katika taarifa ya pamoja kati ya China na Marekani iliyotolewa mwaka 1979, Marekani iliitambua Beijing kama ni serikali pekee halali ya China, ikikubaliana na msimamo wa Wachina kuwa kuna China moja na Taiwan ni sehemu ya taifa hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China amesema kuwa sera inayokubali Taiwan ni sehemu ya China ndio msingi wa uhusiano kati ya Marekani na China na kusisitiza serikali ya Trump “kuelewa umuhimu” wa jambo hili.
Global Times inayodhibitiwa na serikali ilieleza kuwa Trump anaonesha “Si mzoefu” kwa kufikiria anaweza kutumia sera ya Taiwan kulazimisha mazungumzo ya kiuchumi “na anahitaji kujifunza jinsi ya kushughulikia masuala ya mambo ya nje kwa unyenyekevu.”
Gazeti hilo la serikali ya Bejing lilipendekeza kwamba iwapo Trump ataisaidia Taiwan kupata uhuru wake au kuiuziya silaha “hakutakuwa na sababu ya China kushirikiana na Washington katika masuala ya Kimataifa” na itaweza kutoa msaada wa kijeshi na msaada mwengine kwa wapinzani wa Marekani.
Trump atetea mazungumzo yake ya simu
Katika mahojiano na Televisheni ya Fox News Jumapili, Trump aliendelea kutetea mazungumzo yake ya simu na Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen, ambayo ni mawasiliano ya kwanza kati ya kiongozi huyo na Rais wa Marekani au Rais Mteule wa Marekani tangu mwaka 1979, ambapo Marekani iliafiki Taiwan ni sehemu ya umoja wa China.
Vile vile alisema hataki China kumuambia nini lakufanya.
;Sijui kwa nini lazima tulazimike kufuata sera ya China moja isipokuwa labda tukiwa tunataka kufanya makubaliano na China yanayohusu mambo mengine, ikiwemo biashara,” Trump alisema.
Rais-Mteule aliikosoa China kuhusu sera zake za sarafu, na kuongeza nguvu zake za kijeshi katika eneo la South China Sea na kushindwa kwake kuzuia jirani wake Korea ya Kaskazini kufanya majaribio ya silaha za nyuklia.
“Sisi tunaumizwa sana na vitendo vya China kushusha thamani ya sarafu yake ikiwa ni pamoja na kuweka ushuru mkubwa katika mipaka wakati sisi hatuwatozi wao ushuru, na pia kujenga himaya kubwa katikati ya eneo la South China Sea, jambo ambalo hawatakiwi kulifanya, na hawatusaidii kabisa na suala la Korea ya Kaskazini,” Trump alisema.
“Unayo Korea ya Kaskazini. Kuna silaha za nyuklia na China haikuweza kutatua hili tatizo na hawatusaidii kabisa.”
Kauli ya Trump inalenga ushuru wa China na Marekani katika bidhaa zinazouzwa baina yao. China imeweka ushuru wa kati ya asilimia 5 na 9.7 kwa bidhaa za Marekani na Marekani inakusanya asilimia 2.5 na 2.9 ya ushuru.
Trump alisema ingekuwa sio heshima kutokujibu simu ya kiongozi wa Taiwan aliyekuwa anampongeza kwa ushindi wake, akiongeza kuwa alikuwa anaiona number inapiga kwa saa kadhaa na sio kwa wiki au muda mrefu kama vile baadhi ya taarifa za vyombo vya habari vya Marekani zilivyosema.
“Ilikuwa ni mazungumzo mafupi mazuri sana,” alisema Trump. “Na ni kwa nini mataifa mengine yavalie njuga na kusema siwezi kuzungumza na kiongozi huyo.?”
Lakini China imemkosoa Trump kwa hatua ya kupokea simu, lakini walikuwa hawana maelezo ya papo kwa papo kwa kauli yake alioitoa katika mahojiano. Baada ya Trump kuongea na Kiongozi wa Taiwan, Wasemaji wa ngazi za juu wa White House waliwahakishia maafisa wa China kwamba sera ya Marekani ya “China moja” itabakia palepale.
Sihitaji kupashwa taarifa za ujasusi kila siku
Wakati wa Mahojiano, Trump pia alisema hahitaji kupokea taarifa fupi za kintelijensia kila siku akidai kuwa ni zenye kujirudia rudia.
Unajua mimi niko makini, Trump alisema. Sina haja ya kuambiwa kitu kile kile katika maneno yale yale siku baada ya siku kwa miaka 8 ijayo. Inaweza ikawa miaka minane, na sihitaji hilo kwa miaka minane. Lakini ninachosema,”Iwapo kitu kitabadilika tufahamisheni.”
Alisema atapochukua urais rasmi Januari 20, watoto wake wakubwa na viongozi wa kampuni ya Trump wataendesha shughuli za biashara yake duniani na hatojihusisha na uongozi wa biashara hiyo.
Lakini hakusema jinsi atavyokaa mbali na biashara hizo kwani watu wa maadili wanashinikiza afanye hivyo ilikuepuka utata wa maslahi binafsi kwa maamuzi anayoyafanya kama kiongozi wa Marekani.
Trump amepanga kutoa tamko rasmi siku ya Alhamisi juu ya taarifa kamili ya namna atavyo jitenganisha kutoka katika Taasisi ya Trump atapo chukua madaraka.
Amesema kuwa yeye “ni mwazi” katika masuala ya mazingira na iwapo Marekani iendelee kuwafiki makubaliano ya dunia nzima yaliyofikiwa Paris katika kudhibiti gesi za sumu zinazo zalishwa na greenhouse ambazo wanasayansi wamekubaliana yanapelekea katika mabadiliko ya hali ya hewa hatarishi duniani.