Rais wa Uganda Yoweri Museveni na aliyekuwa waziri wake mkuu Amama Mbabazi, wameidhinishwa na tume ya uchaguzi ya Uganda kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
Baada ya kuidhinishwa na tume hiyo, Rais Yoweri Museveni amesisitiza kwamba ameitoa Uganda mbali katika wakati mgumu na huu ndio muda wake kuhakikisha nchi inastawi zaidi.
Bwana Museveni ameongeza kwamba vijana wa sasa wanapaswa kuwauliza wazee kule alikoitoa Uganda.
Naye Waziri Mkuu wa zamani wa Uganda, Amama Mbabazi, amesema kwamba anafahamu siri zote za Museveni, na kuionya tume ya uchaguzi kutofanya udanganyifu wakati wa kuhesabu kura.
Kampeni rasmi zimeanza nchini Uganda baada ya marafiki waliogeuka kuwa wapinzani kisiasa Yoweri Museveni, na Amama Mbabzi kuidhinishwa na tume ya uchaguzi.
Mbabazi na Museveni wamevutia umati mkubwa katika kampeni zao za kwanza ambapo walihutubia wafuasi wao umbali wa kilomita moja kutoka mikutano yao jijini Kampala.
Museveni amesisitiza kwamba hamna anayemzidi ujuzi wa kuongoza Uganda.
Kwa upande wake Bwana Mbabazi alisema Waganda wana kiu cha mabadiliko na wakati wa Museveni kwenda nyumbani uwadia.