Zaidi ya watu 30 wauawa Nairobi

  • Esther Githui-Ewart

Soko kuu la Westgate mjini Nairobi lashambuliwa


Hali ni tete katika jiji la Nairobi ambapo washambuliaji wenye silaha Jujmamosi mchana walivamia eneo la kifahari la Westgate Mall nje kidogo ya jiji la Nairobi.

Vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti kuwa washambuliaji hao waliokuwa waloficha nyuso zao walivamia maduka hayo mwendo wa saa sita mchana kwa saa za Kenya na kuwateka nyara watu kadha.

Wafanyakazi wengi wamenaswa katika mtafaruku huo huku ikiripotiwa kuwa zaidi ya watu 30 wameuawa.Polisi wa Kenya wamewaambia wananchi wasiende eneo hilo ambapo kikosi maalum cha kijeshi KDF kimepelekewa kuwasaka na kukabiliana na washambuliaji hao.

Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika imefanya matangazo ya moja kwa moja saa moja na nusu jioni kwa saa za Afrika Mashariki ambapo mwandishi wetu Mwai Gikonyo, mtangazaji wa televisheni ya K24 TV Franklin Wambugu na mchambuzi wa maswala ya kisiasa na mwandishi wa siku nyingi Kasuja Onyonyi walishiriki na kuelezea matukio hayo ya kusikitisha yaliyokumba jiji la Nairobi.

Polisi huko Nairobi wanasema Westgate Mall sasa imedhibitiwa na kikosi maalum cha kijeshi na kwamba kinafanya upekuzi mkali. Kuna ripoti kuwa mshambualiaji mmoja amekamatwa na msako unaendeela kubaini hasa ni nani waliotekeleza mashambulizi hayo na kwa lengo gani.

Hadi tukienda hewani rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitegemewa kuhutubia Wakenya huku waziri wake wa maswala ya ulinzi wa ndani Joseph Ole Lenku akiwa tayari amezungumza na waandishi habari.

Kwa mujibu wa waandishi habari tuliozungumza nao, viongozi wa Kenya wameonyesha mshikamano wa kitaifa wakati nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikiomboleza maafa yaliyotokea Jumamosi.