Zaidi ya wafungwa dazeni tatu wa Kipalestina wamerejea nyumbani wakipokelewa kishujaa huko Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa kimabavu baada ya kuachiliwa kutoka kwente magereza ya Israel kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.
Msafara wa wafungwa walioachiliwa, wengine wakituhumiwa kwa makosa madogo na wengine waliohukumiwa katika mashambulizi, ulichochea umati mkubwa wa Wapalestina kuimba, kupiga makofi, kupunga mikono, na kuwa na shamrashamra.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na watawala wa Gaza, Hamas yanahusisha kubadilishana, kwa muda wa siku nne, watoto na wanawake 150 wa Kipalestina waliokuwa katika jela ya Israel kwa mateka 50 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas.
Wapalestina wengi wanaotarajiwa kuachiliwa siku zijazo ni vijana waliokamatwa kwa uchochezi na kurusha mawe.