Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Dkt Patrick Otim ambaye ni afisa wa dharura wa WHO amesema kwamba milipuko ya kipindupindu ni hatari kutokana na maambukizi ya haraka pamoja na maeneo yenye maji yaliyosimama.
Amesema ni muhimu kutoa misaada kwa mataifa hayo ili yakabiliane na milipuko kabla haijaenea zaidi. Kufikia sasa kipindupindu kimeripotiwa kwenye mataifa 12 kati ya 54 yaliyopo Afrika. Kesi za karibu zaidi zimeripotiwa Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe. Malawi imeshuhudia mamia ya vifo kutokana na mlipuko unaosemekana kuwa mbaya zaidi nchini humo.
Kisiwa cha Madagascar ambacho kimekumbwa na vimbunga viwili mwaka huu pia kinakabiliwa na mlipuko wa kipindupindu. Kipindupindu ni ugonjwa unaoenezwa na maji machafu, na mkuu wa WHO barani Afrka Dkt Matshidiso Moeti amesema kwamba ongezeko la mvua kwenye mataifa kama Malawi linapunguza juhudi za kudhibiti mlipuko uliopo.
WHO limeonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huenda yakaongeza milipuko ya kipindupindu, kwa kuwa bakteria wanaosababisha ugonjwa huo huzaana kwa kasi zaidi, kwenye maeneo yenye maji yenye joto. Kufikia sasa, chanjo za kumeza kwa mdomo milioni 3.4 zimetumwa Kenya, Congo na Msumbiji, ambako kesi za maambukizi zinaendelea kuongezeka.