Shirika la afya duniani (WHO) limetoa tahadhari dhidi ya matumizi ya dawa mbili za ugonjwa wa kukohoa za India zinazolalamikiwa kusababisha vifo vya watoto wasiopungua 20 nchini Uzbekistan.
WHO imesema bidhaa hizo zilizotengenezwa na kampuni ya Marion Biotech ya India, zilikuwa "chini ya viwango" na kwamba kampuni hiyo imeshindwa kutoa uhakikisho kuhusu "usalama na ubora wake".
Tahadhari hiyo iliyotolewa Jumatano, inakuja baada ya mamlaka ya Uzbekistan kusema mwezi uliopita takriban watoto 20 walifariki baada ya kutumia dawa hiyo ya kunywa na siyo kidonge iliyotengenezwa na kampuni kwa jina Doc-1 Max.
Wizara ya afya ya India baadaye ilisitisha uzalishaji katika kampuni hiyo na Uzbekistan ilipiga marufuku uagizaji na uuzaji wa Doc-1 Max.