WFP inaonya janga la njaa linatarajiwa kutokea nchini Sudan

Wakaazi wa Sudan wakiwemo watoto wakisubiri kupata mgao wa chakula kutokana na vita vinavyoendelea huko. June 16, 2023.

Karibu watu milioni 18 kote Sudan wanakabiliwa na njaa kali hivi sasa, hii ni sawa na idadi nzima ya watu wa Uholanzi, na zaidi ya mara mbili ya idadi hiyo kwa wakati huohuo mwaka mmoja uliopita, msemaji wa WFP nchini Sudan, Leni Kinzli alisema

Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) limeonya kuhusu “janga la njaa” linalotarajiwa kutokea nchini Sudan, ambako miezi kadhaa ya vita, bei ya juu ya chakula na mazao kukauka yameacha idadi kubwa ya watu katika viwango vya dharura vya njaa.

Karibu watu milioni 18 kote Sudan wanakabiliwa na njaa kali hivi sasa, hii ni sawa na idadi nzima ya watu wa Uholanzi, na zaidi ya mara mbili ya idadi hiyo kwa wakati huohuo mwaka mmoja uliopita, msemaji wa WFP nchini Sudan, Leni Kinzli aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano kwa njia ya video kutoka Nairobi.

Mapigano yalizuka kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces, kati-kati ya mwezi Aprili na kuwakosesha makaazi watu milioni 6.6 ndani na nje ya nchi hiyo. Juhudi za mara kwa mara za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano zimeshindwa.