Waziri Mkuu Tanzania ataka hatua zaidi bandarini

Rais wa Tanzania John Magufuli alipohutubia bunge la nchi hiyo.

Serikali mpya ya Tanzania inaendelea na juhudi zake za kupambana na rushwa nchini humo kwa hatua mbali mbali za viongozi wa juu wa nchi hiyo.

rais John magufuli alikutana na wafanyabiashara wakubwa mjini dar es salaam leo na kuwataka wahakiki ulipaji wao kodi – na endapo una mapungufu basi wailipe serikali kodi ambayo hawajalipa.

Your browser doesn’t support HTML5

Ripoti ya Sunday Shomari

Wakat huo huo, Waziri mkuu wa Kassim Majaliwa alifanya ziara nyingine za kushtukiza katika mashirika la bandari na reli mjini dar es salaam na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yaliyotolewa bandarini bila kulipiwa ushuru.

Waziri Mkuu majaliwa alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mamlaka ya bandari mpaka sasa imeachisha kazi watumishi 10 tu kutokana na makosa hayo, hali ambayo haikumridhisha waziri mkuu. “Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu alisema waziri mkuu.

Kutokana na hivyo Waziri Mkuu Majaliwa amemtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga ampelekee majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo ifikapo mwisho mwa siku alhamisi. Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye maandishi ya karatasi na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).

Wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa nepi za watoto lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.

Katika ziara yake katika shirika la reli Waziri Mkuu Majaliwa alikagua mabehewa na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako taarifa ya ofisi ya waziri inasema alibaini ufujaji kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo. “Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema waziri mkuu.

“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh. bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.

Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.

Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Bw.Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.

“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.