Watu zaidi ya 100 wamekufa Nigeria katika mapigano ya wakulima na wafugaji

Mfano wa waandamanaji wakishika mabango huko Nigeria wakipinga mapigano yanayofanyika na kupelekea vifo kati ya wakulima na wafugaji. Nigeria, March 14, 2018.

Mapigano kati ya wafugaji na jamii za wakulima katika jimbo la Plateau ndio mabaya zaidi kutokea katika eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitaabika na mivutano ya kikabila na kidini pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi

Zaidi ya watu 100 kati-kati mwa Nigeria wamekufa katika siku kadhaa za ghasia kati ya jamii mchanganyiko ambazo zimeharibu mamia ya nyumba na kusababisha maelfu kukimbia, maafisa katika eneo wamesema leo Ijumaa.

Mapigano kati ya wafugaji na jamii za wakulima katika jimbo la Plateau ndio mabaya zaidi kutokea katika eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitaabika na mivutano ya kikabila na kidini pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya watu wenye silaha kwenye vijiji vya wakulima ndani na kuzunguka wilaya ya Mangu, tangu mwanzoni mwa wiki imevuka mia moja, baada ya ripoti za awali zilizoeleza watu 85 waliuawa, ofisa mmoja wa eneo hilo alisema.

Vikosi vya usalama vya jimbo la Plateau vilisema Alhamis kwamba hali ya utulivu imerejea, lakini vyanzo katika eneo vilisema vijiji kadhaa bado vilikuwa vikitaabika na ghasia hizo na wakaazi walikimbia.