Hatua hiyo ni sehemu ya kesi ambayo vyombo vya habari vya ndani vimeitaja kuwa inahusiana na tuhuma za njama dhidi ya usalama wa nchi. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wizara ya mambo ya ndani haikujibu maombi ya kuitaka ielezee kuhusu kukamatwa kwa Khayam Turki waziri wa zamani wa fedha, na Kamel Ltaif ambaye mmiliki wa kampuni kubwa ya ujenzi , na mwenye uhusiano wa karibu na serikali kadhaa za muungano zilizoondoka madarakani.
Vyombo vya habari vimeongeza kusema kwamba baadaye polisi walimkamata Abd El Hamid Jlassi afisa wa zamani wa ngazi ya juu kwenye chama cha siasa cha Ennahda Islamist, na pia mkosoaji mkubwa wa rais Kais Saied, akituhumiwa kupanga njama usalama wa nchi. Kituo cha televisheni cha Attessia pamoja na Radio ya Mosaique FM zimesema kwamba afisa mstaafu wa jeshi na ambaye pia ni mwanadiplomasia wa zamani amekamatwa.