Wataalam wasema kwamba kipindupindu kinaenea kwa kasi kubwa DRC

Madaktari wasio na mipaka watengeneza kambi ya kutibu kipindupindu ya Longo, DRC

Wafanyakazi wa misaada Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Alhamisi wameonya kuhusu janga la afya kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya kipindupindu kwenye kambi za muda za wakimbizi.

Madkatari wasio na mipaka maarufu MSF wamesema kwamba kati ya Novemba 26 na Desemba 7, wagonjwa 256 wamelazwa kwenye kituo chao cha afya kilichoko Munigi karibu na mji wa Mashariki mwa Goma.

MSF wameongeza kusema kwamba theluthi moja ya wagonjwa waliofikishwa kituoni humo ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Zaidi ya watu 177,000 sasa hivi wamekwama kwenye kambi za wakimbizi katika hali hatarishi, baada ya kukimbia mashambulizi kutoka kundi la M23 katika wiki za karibuni.

MSF limeongeza kusema kwamba idadi ya maambukizi mapya ya kipindupindu katika siku 10 zilizopita yameongezeka maradufu.