Wasifu wa mgombea nafasi ya urais Yoweri Museveni

Rais Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye hujiita ‘mzee wa Afrika mashariki’ na kuita vijana nchini humo kuwa wajukuu wake yani “bazukulu”, ni mwanasiasa ambaye kila mara hujitambulisha kwa kuvalia kofia ya mviringo.

Alianza siasa akiwa mwanafunzi katika shule ya upili.

Alisomea uchumi na sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Dar-es-Salaam nchini Tanzania.

Alihusika katika kupindua serikali mbili kabla ya kuingia madarakani mwaka 1986.

Alipindua utawala wa Idd Amin (1971 -1971) na Milton Obote (1980 – 1985),

Ametawala Uganda kwa mda wa miaka 34 (January 26, 1986 – 2020) na ana amini kwamba ndiye mtu pekee mwenye uwezo na ujuzi wa kuongoza Uganda.

Museveni anagombea urais kwa mhula wa sita baada ya kufanyia marekebisho katiba ya Uganda mara mbili. Mara ya kwanza mwaka 2005 katiba ilifanyiwa marekebisho na bunge lenye wabunge wengi wa chama cha Museveni cha NRM likaondoa ukomo wa mhula kwa rais. Katiba ilifanyiwa marekebisho mwaka 2018 na kuondoa kizuizi cha miaka kwa wagombea wa urais.

“Utawala wa NRM ndio umetengeneza nchi hii. Natengeneza hali yenu ya baadaye ya kuwa na maisha mazuri” amesema Museveni mara nyingi katika hotuba zake kwa taifa na katika kampeni.

Umri wa Museveni

Museveni ana umri wa miaka 76 lakini suala la umri wake limekumbwa na mjadala. Aliwahi kusema kwamba hajui siku wala mahali alizaliwa. Kumekuwepo kesi mahakamani kuhusu umri wake, lakini anasema alizaliwa Septemba 15 1944.

Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakisema kwamba Museveni amekuwa akidanganya kuhusu umri wake kwa sababu kulikuwepo kizuizi cha umri kwa wagombea wa urais kabla ya katiba kufanyiwa marekebisho

“Wazazi wangu hawakwenda shule, kwa hivyo hawakujua tarehe wala mwezi na mwaka nilipozaliwa.” Aliandika Museveni katika kitabu kuhusu maisha yake, kwa jina Sowing the mustard seed.

Amekuwa akisisitiza kwamba afya yake ni nzuri sana kuongoza taifa. Ili kudhihirisha hilo, amekuwa akifanya mazoezi hadharani n ahata kurekodiwa kwenye video na kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii.

Amesisitiza kwamba hakuna aina yoyote ya mazoezi ambayo hawezi kufanya.

Mara kadhaa, ameambia taifa kwamba hajawahi kulazwa hospitali na kwamba amekuwa tu akitibiwa magonjwa ya kawaida kama malaria, na mafua.

Familia

Rais Yoweri Museveni, kushoto, na mkewe Janet Museveni

Museveni ni baba wa Watoto wanne, mvulana mmoja na wasichana watatu, mzaliwa wa Ntungamo magharibi mwa Uganda.

Mke wake, Jannet Kataha Museveni ni waziri wa elimu. Wameoana kwa mda wa miaka 45.

Museveni aliambia taifa wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake mwaka 2017 kwamba hawajawahi kumpiga mke wake na kwamba mwanamme yeyote anayempiga mkewe ni “mtu mpumbavu sana anayestahili kuadhibiwa mahakamani.”

Wakati mmoja, alisema kwamba kwa miaka yote ambayo ameishi na Janet, hajawahi kumbusu hadharani wala mbele ya Watoto wake.

Tarehe Muhimu katika historia ya Museveni

1944: Mwaka aliozaliwa

1979: Aliongoza mapinduzi kumpindua Idd Amin

1986: Aliingia madarakani kupitia mapinduzi

1996: Alituma wanajeshi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

2001: Aliahidi kutogombea tena urais

2011: Alishinda mhula wa nne madarakani

2016: aligombea mhula wa tano madarakani

2021: Atagombea mhula wa sita madarakani

Makundi ya waasi

Kundi la Lords resistance movement - LRA na allied democratic forces ADF, ni makundi mawili ya waasi ambayo yamekuwa yakipigana vit akupindua utawala war ais Yoweri Museveni.

Kundi la LRA linaongozwa na Joseph Kony.

Kundi la ADF linaongozwa na Jamil Mukulu ambaye alikamatwa nchini Tanzania na anazuiliwa Uganda.

Museveni alianza mashambulizi dhidi ya kundi la LRA mnamo mwaka wa 2004 na kulazimisha kundi hilo kukimbilia Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kufikia mwaka 2006.

Kulingana na ripoti ya shirika la human rights watch (March 21 2012), karibu watu 3000 waliuawa katika mashambulizi ya kundi la LRA, 4000 kutekwa nyara na zaidi ya milioni 1.9 kukoseshwa makaazi.

Mashambulizi ya bunduki yamekuwa yakifanyika katika sehemu mbali mbali za Uganda hasa jijini Kampala yakihusishwa na kundi la ADF.

Kati yam waka 2014 na 2016, viongozi kadhaa wa dini ya kiislamu waliuawa Uganda na mauaji hayo kuhusishwa na kundi la ADF. Polisi walisema kwamba viongozi hao wa kiislamu walikuwa wakiuawa kwa sababu walikataa kushirikiana na kundi la ADF.

Museveni mwanamuziki

Mwaka 2010 Museveni aliimba wimbo ambao ulikuwa maarufu sana kote Afrika mashariki.

Wimbo huo kwa jina ‘anaother rap’ yani ‘wimbo mwingine’ ulitungwa wakati ambapo vijana wengi nchini Uganda walikuwa wanaonyesha dalili za kumuunga mkono aliyekuwa kiongozi wa upinzani wakati huo Dr. Kiiza Besigye.

Dit Kizza Besigye

Another rap maana yake ni kwamba anataka mhula mwingine.

Alikuwa amesema mwaka 2001 kwamba hatagombea mhula mwingine madarakani na kwamba chama cha NRM kilikuwa na viongozi wa kutosha kumrithi. Hajatangaza mpango wowote wa kuandaa mrithi kufikia sasa.

Alimshinda Kiiza Besigye katika uchaguzi huo wa mwaka 2016 kwa asilimia 68 ya kura.

Kuwafunga jela wapinzani wake

Museveni amekuwa rais ambaye karibu wapinzani wake wote wamekamatwa na kufungwa gerezani kwa mda.

Kila mwanasiasa anayemuunga mkono serikalini anakuwa rafiki yake na anayetofautiana naye kimawazo humfuta kazi bila kuchelewa.

Wengi wa wapinzani wake kwa sasa, alikuwa nao katika serikali moja na aliwafuta kazi baada ya kuonyesha dalili za kutaka kugombea urais.

Katika uchaguzi wa mwaka 2006, mpinzani wake mkuu na ambaye alikuwa daktari wake, Dr Kiiza Besigye, alikamatwa na kufunguliwa kesi ya kujaribu kuangusha serikali Pamoja na madai ya ubakaji.

Mashtaka dhidi yake yalitupiliwa mbali na mahakama baada ya kukosekana Ushahidi.

Kila mara Beisgye amekuwa akigombea urais, amekuwa akikamatwa na kufunguliwa mashataka ya kutaka kupindua serikali ya Museveni.

Besigye amejiondoa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2021 na hajakamatwa hata mara moja wala polisi kukita kambi nyumbani kwake ilivyokuwa kawaida wakati anagombea urais.

Aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya Museveni, Amama Mbabazi, naye alikamatwa na polisi alipotangaza kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Mgombea urais wa upinzani Bobi Wine

Mshindani mkubwa wa Museveni katika uchaguzi wa mwaka wa 2021 Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, amekamatwa mara kadhaa. Amefunguliwa mashtaka ya kutaka kupindua rais Museveni. Wafuasi wa Bobi Wine wamepigwa risasi na kuuawa walipoandamana kudai mwanasiasa huyo aachiliwe huru.

Ukuaji wa uchumi na sekta ya elimu kuimarika

Mojawapo ya mafanikio makubwa katika utawala wa miaka 34 ya rais Yoweri Museveni ni kuimarika kwa uchumi ambao ulikuwa umedorora sana chini ya Utawala uliokuwepo kabla yake. Sarafu ya Uganda ilikuwa imekosa thamani.

Idadi ya wanafunzi katika shule za msingi na upili imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Masomo katika shule za msingi na upili ni ya bure. Huduma ya afya ya msingi katika hospitali za uma inatolewa bila malipo.

Museveni amekuwa akijigamba kila mara kwa kuimarisha usalama kote nchini Uganda, jambo ambalo wachambuzi wanasema limechangia sana katika kuendelea kuwepo madarakani.

Idadi ya viwanda na ujenzi wa barabara vimekuwa vikiimaria nchini Uganda.

Uhusiano na na nchi jirani

Wanajeshi wa Uganda walituhumiwa kwa wizi wa mbao na madini katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo mwaka 2000 wakati wanajeshi wa Uganda walipopigana na wa Rwanda nchini humo katika eneo la Kisangani, wakati wa utawala war ais Laurent Kabila.

Uhusiano kati ya Uganda na Rwanda umekuwa mbaya katika siku za hivi karibuni kiasi cha Rwanda kufunga mpaka na Uganda.

Rwanda inadai kwamba Uganda imekuwa ikiwakamata raia wake bila makosa yoyote na kwamba serikali ya Museveni inapanga kupindua itawala war ais Paul Kagame.

Rais Paul Kagame na Rais Yoweri Museveni

Serikali ya Museveni nayo inadai kwamba utawala wa Rwanda umekuwa ukipanga kumpindua Museveni.

Ufisadi serikalini

Kesi za ufisadi zimekuwa zikiripotiwa mara kdhaa nchini Uganda. Hivi karibuni, mgombwa wa urais kupitia chama cha National Alliance and Transformation, ambaye alikuwa kamanda wa jeshi la Uganda Generali Mugisha Muntu, alisema kwamba “ukienda kila mahali hata hospitalini na ikulu yar ais unakutana na ufisadi. Ufisadi upo kila mahali katika serikali hii.”

Museveni ameunda tume tofautikupambana na ufisadi, na hata baadhi ya tume kuongozwa na wanajeshi lakini mafanikio makubwa hayajapatikana.

Mbona Museveni hajakuwa tayari kuondoka madarakani?

Rais Yoweri Museveni, amenukuliwa mara kadhaa na vyombo vya habari kwamba hajamaliza kazi aliyoanza na kwamba ataendelea kuongoza nchi hiyo hadi ndoto yake itakapotimia.

Kazi hiyo ni kuhakikisha Uganda iliyostawi kabisa kiuchumi na kijamii na kuwa miongoni mwa nchi Tajiri duniani, Pamoja na kuhakikisha ndoto ya jumuiya ya Afrika mashariki inatimia na nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan kusini zinashirikiana kabisa katika maswala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Amewahi kushutumiwa na maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi la Uganda kwamba anamtayarisha kijana wake Lt. Gen. Muhoozi Kainerugaba kumrithi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC