Wakati bidhaa kama chakula, maji na dawa zikiendelea kupungua, matumaini yapo kwenye kivuko cha mpakani cha Rafah kati ya Gaza na Msiri, ambako malori yaliyobeba misaada yamekuwa yakisubiri wapatanishi kushinikiza sitisho la mapigano ambalo litawaruhusu wao kuingia Gaza, na kuwaruhusu wageni kuondoka.
Wizara ya afya ya Gaza imesema wapalestina 2,750 wameuwawa huku wengine 9,700 wamejeruhiwa tangu mapigano yalipozuka, ikiwa idadi kubwa kuliko ile ya vita vya Gaza vya 2014 vilivyodumu kwa zaidi wiki 6.
Zaidi ya wa Israeli 1,400 wamekufa, wengi wakiwa raia waliouwawa kwenye shambulizi la Hamas la Oktoba 7. Jeshi la Israel limesema Jumatatu kwamba takriban mateka 199 walipelekwa Gaza wakati wa shambulizi hilo, ikiwa idadi kubwa kuliko makadirio ya awali. Hata hivyo haijabainishwa iwapo kuna raia wa kigeni miongoni mwao.