Wanakijiji 19 wauwawa na wanamgambo mashariki mwa DRC

Wanajeshi wa Congo wakifanya doria katika kijiji cha Mwenda kilichoko Kaskazini Mashariki mwa DRC Mei 23, 2021. Picha na ALEXIS HUGUET / AFP. Picha ya maktaba

Kiongozi mmoja wa asasi za kiraia amesema kwamba wanamgambo wa kiislamu Jumapili jioni wamewafunga kamba wanakijiji 19 na kisha kuwaua kwa kutumia mapanga pamoja na silaha nyingine, katika uvamizi walioufanya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa Mabele Maurice Musaidi kiongozi wa jamii ya kiraia ambaye aliongea na shirika la habari la Reuters, huenda baadhi ya wanakijiji walikufa maji wakati wakijaribu kuvuka mto Lamia wakielekea nchini Uganda.

Musaidi pamoja na msemaji wa jeshi la Congo wamesema kwamba shambulizi hilo kwenye eneo la Beni katika kijiji cha Watalinga limefanywa na waasi wa Allied Democratic Forces, ADF, kundi lenye silaha lenye makao yake mashariki mwa Congo, na ambalo ni tiifu kwa kundi la kigaidi la Islamic State.

ADF lilianzia Uganda kabla ya kuvuka na kuingia nchini DRC katika miaka ya 90, na limelaumiwa kutekeleza maelfu ya mauaji ndani ya muongo mmoja uliopita.

Jeshi la Congo limesema kwamba limewaua wanamgambo nyakati za usiku bila kutoa maelezo zaidi. Msemaji wa jeshi Antony Mualushayi amesema kwamba idadi ya raia waliokufa ni 11, ingawa huenda idadi ikabadilika.