Komanda ni mji mmoja uliopo Kilometa 57 Kusini mwa mji wa Bunia mkoani Ituri ambako maelfu ya wakazi wa eneo hilo wamekimbia na kuhama makazi yao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa waasi wanaodhaniwa kuwa ni ADF.
Manu Mkombozi ni muendesha piki piki na yuko katika mji wa Komanda kukiwa na hali isiyo ya kawaida familia yote ikiwa imeshakimbilia mji wa Bunia.
Ginoce Masumbuko pia ni mkazi wa Komanda anasema hali bado sio nzuri na wakazi wa Irumu hasa eneo hilo linalopakana na wilaya ya Beni Kivu Kaskazini.
Katika wilaya hii imeshuhudiwa waasi wakitokea kila siku na kushambulia wakazi na hata kuchoma nyumba zao na kulazimishwa kuhama nyumba hizo wakikimbilia sehemu salama.
Sauti ya America ilikutana na mama Ubolasu Emerase akiwa na watoto wake wawili pembeni ya barabara akiuza samaki na mboga mboga ,mkazi huyo anasema mjini hakuna watu, Mbuzi wala kuku wote weshakimbia kunusuru maisha yao.
Mkazi mwingine Kambale kataliko anasema ameshindwa kuendelea na safari kutoka Bunia kwenda Butembo akisema ameambiwa njia haina usalama.
Baadhi ya miji wilayani Irumu na Djugu inakabiliwa na mashambulIzi ya waasi wanaodhaniwa kuwa ni ADF wakilazimisha wakazi kuhama nyumba zao na kuwa wakimbizi na kulazimisha vijana kuanza kulinda vijiji vyao kuliko kuviacha katika mikono ya waasi wa ADF kama Mji wa Komanda ambako kuna ulinzi wa vijana wa Chini ya Kilima.
Imeandaliwa na Austere Malivika Sauti ya Amerika-Goma