Wafanyakazi wa Nigeria wafanya mgomo kulalamikia gharama ya maisha

Wafanyakazi kutoka muungano wa Nigeria Labour Congress, NLC, wakiwa kwenye maandamano mjini Lagos. Picha ya maktaba. Julai 26, 2022.

Baadhi ya wafanyakazi katika ofisi za serikali nchini  Nigeria Jumanne waliondoka kwenye maeneo ya kazini kupinga  kupanda kwa  gharama ya maisha kutokana na kuondolewa ruzuku ya mafuta, wakitishia kusimamisha shughuli katika nchi hiyo ya Afrika yenye uchumi mkubwa zaidi .

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, maelfu ya wafanyakazi kutoka chama cha wafanyakazi cha Nigeria Labor Congress walianza mgomo wa siku mbili, wakisema ni “onyo kwa serikali” ukiwa wa pili chini ya miezi miwili. Wiki iliyopita walikutana na kulalamikia hatua ya Rais wa Nigeria Bola Tinubu kuondoa ruzuku za mafuta hapo Mei, hatua iliyosababisha hali ngumu ya kiuchumi kwa wafanyakazi wa taifa hilo pamoja na umma kwa jumla.

Vyombo vya habari vya ndani vimesema kwamba wawakilishi kadhaa kutoka vyama tofauti vya wafanyakazi waliomba wanachama wao wasiende kazini huku baadhi wakifunga ofisi za serikali ili kuhakikisha wameshiriki kwenye mgomo. Hata hivyo mgomo huo haukutekelezwa kote nchini kwa viwango vilivyotarajiwa.

Juhudi za kuzuia mgomo zilishindikana Jumatatu jioni baada ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi kukataa kuhudhuria mkutano ulioitishwa na wizara ya kazi. Rais wa chama cha wafanyakazi Joe Ajaero amesema kwamba wataliunga taifa kwa muda usiojulikana katika muda wa wiki mbili zijazo, iwapo serikali haitatimiza matakwa ya wafanyakazi ikiwemo nyongeza ya mishahara.