Maafisa usalama wa Ethiopia Jumatatu waliwazuia waandishi wa habari kusafiri kuelekea mkoa wa kaskazini wa Tigray kuripoti uchaguzi wa mkoa ambao serikali imeuita kuwa ni kinyume cha katiba. Viongozi pia walichukua simu za mkononi, kompyuta, hati za kusafiria na vitambulisho vya uandishi kutoka kwa waandishi hao.
Uchaguzi uliopangwa Septemba tisa umeitia wasi wasi serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed wakati anajaribu kuibadilisha nchi hiyo kuingia katika enzi mpya ya uwazi zaidi.
Eneo la Tigray, ambalo liliongoza umoja wa serikali ya vyama vingi kwa miaka 27 kabla ya Abiy kuingia madarakani, lilipinga vikali uamuzi wa serikali mnamo mwezi Machi kuahirisha uchaguzi wa kitaifa kwa sababu ya virusi vya corona. Imeliita jaribio lolote la kuzuia kura yake ya kikanda kufanyika ni tamko la vita.
Baraza kuu la bunge la Ethiopia Jumamosi liliita uchaguzi wa Tigray kuwa haramu lakini likaacha kutoa mapendekezo ya vikwazo vyovyote kwa mkoa huo ikiwa wataendelea mbele na uchaguzi.
Makundi ya haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari yalilaani unyanyasaji wa waandishi wa habari kwa kusema ni muhimu sana kwa vyombo vya habari vya kimataifa na vya ndani kuripoti jambo kama la uchaguzi wa Tigray,
“Matukio katika mkoa wa Tigray yanavutia sana umma hivi sasa. Serikali kuu haipaswi kuwazuia waandishi wa habari, iwe ni waandishi wa habari wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari vya kimataifa au vya Ethiopia juu ya uwezo wa kuripoti kwa uhuru juu ya maendeleo haya ya kisiasa.” alisema Laetitia Bader, mkurugenzi wa Pembe ya Afrika katika shirika la Human Rights Watch alipozungumza na VOA.
Wakati wanakaribia mlango wa kupita kwenda kupanda ndege kuelekea Mekele, waandishi wa habari na abiria wengine kadhaa, ikiwa ni pamoja na William Davison kutoka International Crisis Group, waliulizwa na maafisa wawili wa usalama ambao walikuwa wakifanya kazi, kwanini walikuwa wakisafiri kwenda Mekele na nini ilikuwa sababu ya safari yao.
Wanahabari watatu wa eneo hilo wanaofanya kazi kwenye shirika la habari la Awlo na vile vile mwandishi wa VOA walinyang'anywa simu zao, pasipoti na vitambulisho vya uandishi wa habari. Afisa mmoja pia alichukua nambari za simu kutoka kwa simu ya waandishi hawa na kuchunguza akaunti za mitandao yao ya kijamii.
Wanahabari wawili kutoka shirika la Awlo waliohojiwa katika eneo hilo walisema walizuiwa kusafiri kutokana na uchaguzi huko Mekele. Wiki iliyopita, Mamlaka ya Utangazaji ya Ethiopia ilitoa wito kwa waandishi kadhaa wa habari na kuwaonya kutoripoti upigaji kura kwa madai kwamba hautambuliki na serikali kuu.
Msemaji wa ofisi ya waziri mkuu alikataa kutoa maoni yake na maafisa wa Wizara ya Mambo ya nje hawakuweza kufikiwa mara moja. Chama cha Waandishi wa Habari wa Kigeni wa Ethiopia kilisema kilikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya majaribio ya kuwazuia waandishi wa habari kuripoti uchaguzi huko Tigray.
Tunatoa wito kwa maafisa wa serikali kuu ya Ethiopia wasidharau hatua muhimu zilizochukuliwa kuongeza uhuru wa vyombo vya habari katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kwa kujaribu kufuatilia ni kitu gani waandishi wa habari wanaweza au hawawezi kuripoti, FCA ilisema katika taarifa yake.