Waandamanaji Bangladesh wamewashambulia wafuasi wa Hasina

Baadhi ya waandamanaji katika mitaa nchini Bangladesh

Waliwashambulia wafuasi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu Hasina na kuwazuia kufika kwenye nyumba ya awali ya baba yake.

Mamia ya waandamanaji wanafunzi na wanaharakati wa kisiasa nchini Bangladesh, wakiwa wamejihami kwa kutumia fimbo za mianzi, mawe na mabomba ya chuma, leo Alhamisi waliwashambulia wafuasi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu Sheikh Hasina na kuwazuia kufika kwenye nyumba ya awali ya baba yake na muasisi wa uhuru aliyeuawa katika mji mkuu, Sheikh Mujibur Rahman.

Nyumba hiyo iliyoko eneo la Dhanmondi mjini Dhaka iligeuzwa kuwa jumba la makumbusho ili kuonyesha simulizi na vitu vingine kuhusu mapinduzi ya kijeshi mnamo Agosti 15, 1975 wakati Rahman alipouawa pamoja na watu wengi katika familia yake. Nyumba hiyo ambayo kwa sasa inaitwa Bangabandhu Memorial Museum ilichomwa moto na waandamanaji baada ya kujiuzulu kwa Hasina Agosti 5 kufuatia uasi ambapo zaidi ya watu 300 waliuawa.