Wanamgambo wa ki-Houthi nchini Yemen wamesema Jumatano kuwa walirusha makombora kadhaa katika meli ya kivita ya Marekani katika bahari ya Sham na kwamba wanapanga kuendelea kuzilenga meli za Marekani na Uingereza.
Taarifa hiyo imekuja saa chache baada ya jeshi la Marekani kusema kuwa meli ya USS Gravely iliangusha kombora la kuishambulia meli ya kivita iliyorushwa kutoka Yemen na waasi wa ki-Houthi wanaoungwa mkono na Iran.
CENTCOM imesema katika taarifa yake kwamba hakuna majeruhi wala uharibifu wowote, uliotokana na shambulio hilo. Waasi wa ki-Houthi wamefanya mashambulizi zaidi ya 30 ya makombora na ndege zisizokuwa na rubani katika bahari ya Sham tangu kati-kati ya mwezi Novemba, na kusababisha usumbufu mkubwa kwa meli za kibiashara katika njia hiyo muhimu ya majini.