Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, baadhi ya wagombea hao wanadai kuwa kucheleweshwa kwa uchaguzi wa Jumatano huenda kukapelekea udanganyifu, pamoja na kushuka kwa hadhi ya zoezi hilo.
Mara nyingi mivutano ya uchaguzi hupelekea ghasia nchini Congo, kukiwa na hatari ya kuyumba kwa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini, na ambalo tayari linakabiliwa na umasikini mkubwa, pamoja na ukosefu wa usalama upande wa mashariki.
Wagombea watano wa upinzani wanapanga kuitisha maandamano ya Decemba 27, kulingana na barua ya Desemba 22 kwa gavana wa Kinshasa, iliyowekwa kwenye ukurasa wa X, na Jean-Marc Kabunda ambaye ni mwakilishi wa mmoja wa wagombea wa urais Martin Fayulu.
“Tutalalamikia dosari zilizojitokeza wakati wa kupiga kura na hata kabla. Pia tutalalamikia kucheleweshwa kwa zoezi hilo,” imeongeza barua hiyo.