Mkuu wa baraza jipya la utawala Burkina Faso alisema Rais na Waziri Mkuu wapo salama chini ya ulinzi wa jeshi na karibuni wataachiwa.
Brigedia Jenerali, Gilbert Diendere alizungumza na Sauti ya Amerika hapo Alhamis, siku moja baada ya wanajeshi kuiangusha serikali ya muda kwenye taifa la Afrika magharibi na kuwakamata viongozi wake. Jenerali huyo alisema jeshi lilipanga mapinduzi kwa sababu utaratibu wa kisiasa nchini humo haukuwa wa haki.
Alisema ataanza mashauriano ya kisiasa yanayojumuisha pande zote. Burkina Faso ilipanga kufanya uchaguzi wa urais na bunge hapo Oktoba 11. Tarehe hiyo hivi sasa ipo njia panda.
Watu wasiopungua watatu waliripotiwa kuuwawa wakati waandamanaji vijana walipojaribu kukusanyika karibu na makazi ya rais huko Ouagadougou na ubalozi wa Marekani ulisema vizuizi vya barabarani vimewekwa kote mjini humo.
White House mjini Washington ililaani vikali kile ilichokiita jaribio ambalo ni kinyume cha katiba la kuchukua madaraka. Naibu msaidizi wa Umoja wa Afrika, Erastus Mwencha aliwataka Alhamis viongozi hao wa kijeshi haraka kukabidhi madaraka kwa serikali ya muda. “Serikali yeyote ambayo haifuati katiba inalaumiwa moja kwa moja kwa sababu tunaamini katika utawala wa sheria na mabadiliko yeyote ya madaraka lazima yafuate utaratibu wa katiba”, alisema Mwencha.
Pia aliwasihi watu kutoshirikiana na jeshi kuchukua madaraka.
Serikali ya muda ilichukua madaraka nchini Burkina Faso wakati ghasia maarufu zilizomuondoa Rais Blaise Compaore madarakani mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kuwepo mamlakani kwa miaka 27. Alipanga kubadili katiba ili aweze kuongeza utawala wake.