Viongozi wa Japan na Korea Kusini kukutana na Biden katika Camp David, Maryland, mwishoni mwa wiki

Rais wa Marekani Joe Biden na mke wake Jill Biden wakiwasili Camp Biden

Maafisa wa Marekani pamoja na wachambuzi wamesema kwamba viongozi wa Marekani, Japan na Jamhuri ya Korea wanalenga kuimarisha ushirikiano wao kupitia kikao cha kila mwaka wakati tishio kutoka Korea Kaskazini na China likiendelea kuongezeka.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken Jumanne amefanya mkutano wa kimitandao na wenzake wa Japan na Korea Kusini siku chache kabla ya rais wa Merakani Joe Biden kuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Japan Kishida Fumio na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeo kwenye makao ya Camp David hapa Marekani Ijumaa.

Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi wa kigeni kukutana Camp David kwenye jimbo la Maryland tangu 2015, pia kikiwa kikao cha kwanza cha kipekee kati ya mataifa matatu mbali na vikao vikubwa vya kimataifa.

Blinken wakati akizungumza na wanahabari Jumanne alisema kwamba mkutano wao huenda ukaangazia masuala kama vile usalama wa kieneo, usalama wa kiuchumi, misaada ya kibinadamu na teknolojia ibuka miongoni mwa mwengine.