Wakati kukiwa na shinikizo la kimataifa la kusitisha mapigano kwa muda katika Ukanda wa Gaza, vikosi vya Israel vilifanya mashambulizi ya anga Jumatano huko kaskazini na kusini mwa Gaza.
Mashambulizi ya Israel yalijumuisha Gaza City, ambako jeshi limesema pia liliwaua wanamgambo 15 wakati wa oparesheni za ardhini. Katika mji wa Khan Younis, mji mkuu kusini mwa Gaza, mashahidi waliripoti kuwepo mapigano makali pamoja na mashambulizi kadhaa ya anga.
Wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya Israel imeongezeka hadi 26,900, idadi ambayo inajumuisha raia na wanamgambo.
Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh alitarajiwa kusafiri kwenda Cairo kujadili pendekezo la kusitisha mapigano, ambalo litajumuisha vyote kusitisha mapigano katika Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas.