Utafiti unaonyesha chanjo ya Pfizer ina ufanisi wa asilimia 90

Mfanyakazi wa afya Chanjo ya Pfizer ya kupambana na corona akiandaa chanjo hiyo.

Utafiti mpya unaonyesha chanjo ya dozi mbili ya COVID-19 iliyotengenezwa na Pfizer na BioNTech ina ufanisi wa asilimia 90 kumzuia mtu kulazwa hospitali

Utafiti mpya unaonyesha chanjo ya dozi mbili ya COVID-19 iliyotengenezwa na Pfizer na BioNTech ina ufanisi wa asilimia 90 kumzuia mtu kulazwa hospitali kutokana na virusi hadi miezi sita baada ya kupokea dozi ya pili.

Watafiti kutoka Pfizer na ushirika wa huduma za afya Marekani, Kaiser Permanente walichunguza rekodi za watu wapatao milioni 3.4 ambao walikuwa wanachama wa bima ya afya ya Kaiser huko Kusini mwa California na mpango wa kutoa huduma kati ya Desemba 2020 na Agosti mwaka huu.

Utafiti huo, uliochapishwa Jumatatu katika jarida la afya la Lancet, pia ulifafanua kwamba chanjo hiyo ilikuwa na ufanisi wa asilimia 93 dhidi ya aina mpya inayoambukiza sana ya Delta kwa angalau miezi sita baada ya chanjo ya pili.

Lakini watafiti pia waligundua kuwa ufanisi wa chanjo dhidi ya maambukizi ulipungua kutoka asilimia 88 mwezi mmoja baada ya kumaliza hadi asilimia 47 baada ya miezi sita.