Jumamosi iliopita serikali ililaumu aliekuwa rais wa taifa hilo Francois Bozize kwa kupanga kupindua serikali baada ya kunyimwa nafasi ya kuwania kiti cha urais. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mapigano yamekuwa yakiendelea kwenye miji kadhaa uliwemo ule wa Mbaiki ulioko takriban kilomita 100 kutoka Bangui.
Muungano wa upinzani unaojulikana kama Cod2020, na ambao Bozize ni mwanachama unadai kuwa ghasia zimezuia wagombea wa urais na ubunge kufanya kampeni zao. Wanasema kuwa vifaa muhimu vya kampeni pia vimeharibiwa kwenye ghasia hizo wakati pia kukiwa na madai ya kutishiwa maisha.
Kupitia taarifa ya pamoja wamesema kuwa zoezi la uchaguzi haliwezi kufanyika kamwe kwa mazingira yaliopo nchini.
Mtayarishi: Harrison Kamau