Upinzani nchini Zimbabwe umekwenda mahakamani kulalamikia ukandamizaji wa serikali

Wafuasi wa kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe Nelson Chamisa. Mei 30. 2023

Chama kikuu cha upinzani cha Zimbabwe Jumamosi kimekwenda mahakamani kupinga uamuzi wa polisi wa kupiga marufuku mkutano wa kisiasa uliopangwa kabla ya uchaguzi mkuu unaofuatiliwa kwa kina, kufanyika mwezi ujao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, chama cha Citizens Coalition for Change, kimeambiwa kwamba hakiwezi kufanya mkutano Jumapili, kwenye mji wa kaskazini mwa Harare wa Bindura. Polisi wamedai kuwa mji huo huo hauna miundo mbinu ya kutosha kama vile barabara miongoni mwa mengine, kuruhusu mkutano huo kufanyika.

Chama hicho kimedai kwamba hatua hiyo ni mfano mwingine wa nammna utawala wa Rais Emmerson Mnangagwa unavyokandamiza upinzani kabla ya uchaguzi wa Agosti 23. Taifa hilo la kusini mwa Afrika lina historia ya ghasia na mivutano baada ya uchaguzi, ikiwemo miaka mitano iliyopita, pale Mnangagwa aliposhinda kwa kura chache, baada ya kumuondoa madarakani kupitia mapinduzi, rais wa muda mrefu Robert Mugabe.