Umoja wa Mataifa ulisema Jumatano kwamba walinda amani waligundua makaburi ya halaiki mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mfululizo wa mashambulizi yanayolaumiwa kufanywa na wanamgambo wa eneo hilo.
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari kaburi moja katika kijiji cha Nyamamba lilikuwa na miili 42 wakiwemo watoto sita. Miili saba iligunduliwa katika kaburi moja kwenye kijiji cha Mbogi.
Makaburi hayo yapo katika jimbo la Ituri, ambako Haq alisema hali ya usalama imedorora katika maeneo ya Djugu na Mahagi.
Haq alisema tangu mwezi Disemba,vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vimesema takriban raia 195 wameuawa na watu 84 kutekwa nyara katika matukio yanayohusishwa na makundi mawili yenye silaha ya CODECO na Zaire.
Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni 1.5 wameyakimbia makaazi yao huko Ituri na mashambulizi hayo yamekwamisha juhudi za kibinadamu.