Ukraine yadai Russia imetuma ndege zizizo na rubani kwenye uwanja wa vita

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy

Ukraine imesema Jumatano kwamba Russia imetuma  ndege zisizo na rubani  14 pamoja na makombora ya masafa marefu kama sehemu ya mashambulizi yake ya karibuni.

Jeshi la anga la Ukraine limesema kwamba limezitungua droni zote ambazo zilielekezwa sehemu za kati, kusini mashariki na magharibi mwa Ukraine. Hata hivyo hakuna ripoti zozote za uharibifu mkubwa au vifo. Jeshi hilo pia limesema kwamba kombora la Russia aina ya X-22 lilianguka karibu na uwanja katika mkoa wa Zaporizhia bila kufika lilikoelekezwa.

Ukraine imezitambua droni hizo za Russia kuwa ni aina ya Shahed zilizotengenezewa Iran, na mashambulizi hayo yanafuatia maonyo ya Marekani kwamba huenda Iran inaipatia Russia makombora ya masafa marefu kwa ajili ya kutumika katika vita nchini Ukraine.

Msemaji wa baraza la usalama la taifa la Marekani John Kirby amesema kwamba mbali na droni, Iran pia imeipatia Russia mabomu pamoja na silaha nyingine ili zitumike dhidi ya Ukraine.