Jeshi la anga la Ukraine limesema kwamba droni hizo zimeharibiwa kwenye mikoa kadhaa, ikiwemo Odesa, Kherson, Mykolaiv na Donetsk. Gavana wa mkoa wa Odesa, Oleh Kiper amesema kupitia ujumbe wa Telegram kwamba droni 17 zimeangushwa huko, mabaki ya moja ya droni hizo ikiharibu miundo mbinu ya bandari huko Odesa.
Jeshi la Ukraine pia limeripoti kuharibu makombora mawili ya Russia. Katika hotuba yake ya usiku kwa taifa kwenye mkesha wa Krismasi, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema kwamba Krismasi ya mwaka wa pili mfululizo wakati wa vita vya Russia dhidi ya Ukraine, kilicho muhimu kwa familia za Ukraine siyo chakula kilichopo mezani, bali ni watu waliopo kwenye meza, na thamani yao kuwepo.
Amesema kwamba Imani na matarajio ya watu wa Ukraine yamebadilika tangu kuanza kwa vita hivyo. Kwa mara ya kwanza tangu 1917, Ukraine inasherehekea Krismasi Desemba 25, kinyume na Januari 7, tarehe ambayo Russia husherehekea.