Uingereza na Norway zimetangaza Jumatatu kuwa zinashirikiana kuimarisha jeshi la majini la Ukraine, ikisema kuwa vikosi vya majini vyenye nguvu ni muhimu katika kukabiliana na uchokozi wa Russia na kuhakikisha usafirishaji wa nafaka na chuma kupitia Black Sea.
Kama sehemu ya juhudi, Uingereza inatuma meli mbili za kufuatilia silaha, magari ya kivita na boti za uvamizi wa pwani kwenda Ukraine, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Grant Shapps alisema.
Shapps na waziri wa ulinzi wa Norway, Bjorn Arild Gram walitangaza kuundwa kwa muungano wenye uwezo wa baharini wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini London, akisema mataifa mengine yalitarajiwa kujiunga hivi karibuni, na kulifanya kuwa suala linalogusa ulimwengu.
Ahadi ya Ulaya kwa Ukraine kutokana na uvamizi wa Rais wa Russia Vladimir Putin bado ni imara, licha ya hofu kwamba ufadhili waMarekani utasitishwa kutokana na mzozo wa kisiasa katika Bunge.