Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema Jumamosi kwamba Russia "ina uwezekano mkubwa" ilipata maafa kwa wanajeshi zaidi ya 300 katika shambulizi la siku ya mwaka mpya kwa wanajeshi wake nchini Ukraine huko Makiivka karibu na Donetsk City.
Wizara hiyo imesema inaamini kwamba "wengi huenda waliuawa au kupotea, zaidi ya kujeruhiwa".
Wizara hiyo ilibaini kuwa wakati mwenzake wa Russia "alichukua hatua nadra ya kukiri hadharani" kwamba wamepata majeruhi, Russia ilidai ni watu 89 pekee waliouawa.
Wizara ya Uingereza imesema wizara ya Russia "huenda ilifanya tathmini" kuwa haiwezi kuepuka kuzungumzia shambulio hilo kwa sababu makamanda wa Russia wamekuwa wakikosolewa vikali kufuatia tukio hilo.
Wizara ya Uingereza ilisema katika taarifa yake mpya ya kijasusi iliyochapishwa kwenye Twitter kwamba tofauti kati ya idadi ya majeruhi wa Russia na idadi ya kweli "inaonyesha uwepo mkubwa wa habari za kupotosha katika matangazo ya umma ya Russia".