Uholanzi, Brazil zashinda

Luis Fabiano, Kaka na Daniel Alves wakishangilia bao la pili kwenye ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Chile kwenye uwanja wa Ellis Park huko Johannesburg, Afrika Kusini.(AP Photo/Ivan Sekretarev)

Timu za Uholanzi na Brazil zimefanikiwa kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya kombe la dunia baada ya kushinda mechi zao.

Timu ya Uholanzi imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya kombe la dunia baada ya kuifunga Slovakia mabao 2-1.

Mabao ya Uholanzi yalifungwa na Arjen Robben na Wesley Sneijder. Arjen Robben alikosa mechi mbili za awali kutokana na maumivu ya misuli ya paja.

Slovakia walipata bao la kufutia machozi baada ya golikipa wa Uholanzi Maarten Stekelenburg kumwangusha mshambuliaji wa Slovakia Martin Jakubko katika eneo la hatari na kupata penalti ambapo mshambuliaji hatari wa Slovakia Robert Vittek aliweka mpira wavuni.

Nao Brazil waliwafungisha virago Chile kwenye mechi ya pili baada ya kuwabwaga kwa mabao 3-0 mabao ya Brazil yalifungwa na Juan, Luis Fabiano na Robinho.

Chile walikosa nafasi kadhaa lakini kubwa zaidi ilikuwa kunako dakika ya 78 ambapo mshambuliaji hatari Suazo alipodokoa mpira kwenye lango la Brazil ambao ulienda kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.

Hivi sasa timu zinapumzika mpaka Ijumaa ambapo Brazil watafungua dimba la robo fainali na Uholanzi nao wawakilishi pekee wa Afrika Ghana watapambana na Uruguay katika mechi ya pili.

Na siku ya Jumamosi mechi ya kwanza itakuwa kati ya Argentina na Ujerumani na mechi ya pili mchana huo ni kati ya Hispania na Paraguay.