Wizara ya mafuta ya Uganda imesema Jumamosi kwamba imeongeza muda wa leseni kwa kampuni ya Nigeria ya Oranto Petroleum Limited, kwa muda wa miaka miwili zaidi.
Hatua hiyo sasa itatoa nafasi kwa kampuni hiyo kuendelea kutafuta mafuta kwenye maeneo mawili yaliopo magharibi mwa nchi. Leseni hiyo inayojumuisha maeneo ya Ngassa Deep na Ngassa Shallow itaruhusu kampuni hiyo kutafuta na kuidhinisha shuguli za uchimbaji mafuta, kulingana na taarifa iliyotolewa Ijumaa jioni.
Uganda iligundua mafuta yanayofikia viwango vya kibiashara kwenye eneo la Albertine Graben, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hapo 2006, wakati ikipanga kuanza kuyauza kufikia 2025.