Mamlaka ya Ufaransa inasema msichana mwenye umri wa miaka 7 alikuwa miongoni mwa wahamiaji watano waliozama kwenye mfereji wa bahari kati ya Uingereza na Ufaransa, maarufu English Channel, siku ya Jumanne saa chache baada ya wabunge wa Uingereza kupiga kura kupitia sheria inayolenga kuwazuia wanaotafuta hifadhi kuvuka katika eneo hilo.
Maafisa wa eneo hilo walisema boti hiyo iliyokuwa imebeba watu 112 iligonga kwenye ukingo wa mchanga baada ya kuondoka katika ufuo wa bahari karibu na kijiji cha Wimereux.
Mita mia chache kutoka ufukweni, injini ilisimama, na watu kadhaa wakaanguka ndani ya maji," alisema Jacques Billant, gavana wa eneo la Pas-de-Calais la Ufaransa.
"Licha ya hali hii tata na yenye utete, watu 57 ambao walikuwa bado kwenye boti hiyo walibaki ndani. Hawakuwa tayari kuokolewa, walifanikiwa kuwasha tena injini yake na kuamua kuendelea na safari yao ya baharini kuelekea Uingereza,” Billant aliwaambia waandishi wa habari.
Ndivyo azma ya wahamiaji hao kufikia ufuo wa Uingereza. Zaidi ya watu 6,300 wamesafiri kupitia mfereji huo unaogawa Uingereza na Ufaransa kwa boti ndogo kufikia sasa mwaka huu.
Mkasa huo ulitokea mapema Jumanne asubuhi, saa chache baada ya wabunge wa Uingereza kupitisha sheria ambayo serikali inatumai itairuhusu kuwafukuza wanaotafuta hifadhi wanaofika kwa boti ndogo kupitia mfereji huo hadi Rwanda kwa ajili ya kupewa hifadhi.