Ufaransa inailaumu Rwanda kwa tuhuma za kuunga mkono waasi wa M23 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye jimbo lenye migogoro ambako wanamgambo hao wameteka maeneo mengi katika miezi ya karibuni.
Wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa DRC wa Kinshasa siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Chrysoula Zacharopoulou aliwaambia waandishi wa habari kwamba kundi la M23 lazima liweke silaha chini na kuondoka kutoka maeneo inayoyakalia.
"Rwanda, kwa sababu lazima itajwe, lazima iache kuunga mkono M23," alisema. "Lazima tukomeshe historia inayojirudia katika eneo hili".
Tamko la Zacharopoulou limetolewa baada ya wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, siku ya jumatatu jioni pia ili-itaka Rwanda kuacha uhusiano na kundi la M23.
Kundi hilo la waasi linaloongozwa na Watutsi la M23 lilijizolea umaarufu kwa mara ya kwanza wakati lilipouteka mji wa mashariki mwa Congo wa Goma mwaka 2012 kabla ya kufurushwa na kwenda mafichoni