Tshisekedi atangazwa mshindi wa Urais kwa muhula wa pili nchini DRC

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi.

Rais wa Congo Felix Tshisekedi amechaguliwa tena kwa muhula wa pili baada ya kujipatia zaidi ya asilimia 73 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi mkuu wa Desemba 20, tume ya uchaguzi ya CENI imetangaza  Jumapili.

Wakati wa kutolewa kwa tangazo hilo, kwenye mji mkuu wa Kinshasa mwenyekiti wa tume hiyo Denis Kadima ameseama kwamba Tshisekedi amepata asilimia 73.34 ya kura milioni 13 zilizopigwa kutoka kwa jumla ya wapiga kura milioni 18 waliojiandikisha nchini humo. Awali kundi la wagombea urais kutoka upande wa upinzani kwenye uchaguzi huo waliomba wafuasi wao kujitokeza mitaani, ili kupinga matokeo ya awali ya zoezi hilo lililozua utata.

“ Tunapinga vikali uchaguzi huo bandia na matokeo yake,” wagombea wakuu wa upinzani walisema kupitia taarifa ya pamoja, wakidai kufanyika kwa uchaguzi mpya utakaosimamiwa na tume mpya ya uchaguzi, katika tarehe watakayokubaliana wote. “Tunaomba watu wajitokeze kwa wingi barabarani ili kupinga uchaguzi huo wenye udanganyifu,” taarifa yao imeongeza.