Rais wa Marekani, Donald Trump amewataka viongozi wa dunia waliokusanyika kwa ajili ya mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa “kuutenga utawala wa Iran kutokana na kuendeleza uchokozi wake,” na kuwashutumu wa Iran kwa kupanda mbegu za “vurugu, vifo na uharibifu.”
“Hawaheshimu majirani zao au mipaka au haki za utaifa wa mataifa mengine. Badala yake, viongozi wa Iran wanavuruga rasilimali za taifa kwa kujilimbikizia utajiri na kusambaza vurugu kote katika eneo la Mashariki ya Kati na mbali ya huko,” Trump amesema katika hotuba yake Jumanne kwa baraza kuu.
Trump amesisitiza kwamba makubaliano yaliyofikiwa enzi ya utawala wa Obama mwaka 2015 ya kuitaka Iran kumaliza program zake za silaha za nyukli, ambapo yeye amejitoa, ilikuwa ni “mpango kwa viongozi wa Iran na kuboresha bajeti ya jeshi lake kwa karibu asilimia 40 ili ‘kufadhili ugaidi na kufadhili vurugu na kufanya mauaji nchini Syria na Yemen.”
Rais amesema utawala wake ulianza mwezi uliopita “kuweka vikwazo vikali vya nyuklia ambavyo viliondolewa wakati wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa na Iran” na kwamba vikwazo zaidi huenda vikawekwa hapo Novemba 5 au baada ya muda huo.
“Hatuwezi kuruhusu mfadhili mkuu wa ugaidi duniani kuwa na silaha hatari katika dunia hii. hatuwezi kuruhusu utawala ambao unapiga kelele za vifo kwa Marekani na kwamba wanaitishia kuingamiza Israel,” amesema Trump.
Baadaye akiongea na wana habari wakati akiwa pamoja na rais wa Colombia, Ivan Duque, Trump amesema: “Nina matumaini kuwa tunaweza kuwa na mipango” na Iran kama ile ambayo Marekani iliyonayo na Korea Kaskazini.
“Mimi ndiye niliyesema siyo wa,” kuhusu kukutana na maafisa wa Iran wakati wa mkutano wa UN. Trump ameongezea kuwa mazungumzo kama hayo hayawezi kutokea mpaka Tehran ibadili mwenendo wake.
“Vinginevyo wanaweza kuingia katika matatizo makubwa nan chi yoyote duniani,” amesema rais wa Marekani.
Mapema Jumanne, Trump aliandika kwenye Twitter kuwa amekataa maombi kadhaa ya kukutana na rais wa Iran, Hassan Rouhani, jambo ambalo Rouhani amelikanusha vikali.
“Si mwaka huu, wala si mwaka jana " Rouhani amekiambia kituo cha televisheni cha CNN hatujawahi kuwasilisha ombi kama hilo la kutaka mkutano na rais wa Marekani.”
Mapema mwaka huu, Trump alitangaza kuwa Marekani inajiondoa kutoka kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran. Mwezi Novemba, makampuni yanayofanya biashara na Iran yanatakiwa kusitisha biashara zao au yatakabiliwa na hatari ya kufungiwa mifumo yao ya fedha nchini Marekani. Washington inataka kuishinikia Tehran kurejea kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya makubaliano mapya.